Ligi Kuu

Mangungu: Simba haina Mtendaji Mkuu

DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, amesema Simba Sports Club haina Mtendaji Mkuu, kuwa nafasi hiyo inahusishwa na kampuni ya Simba Sports Club, ambayo ina muundo wake wa uendeshaji.

Mangungu amesema kuna tofauti kati ya Simba Sports Club na Simba Sports Club Company, akibainisha kuwa watu wawili wanaohusishwa na nafasi za uongozi wa kiutendaji wamesajiliwa na mamlaka tofauti, mmoja na Baraza la Michezo ya Tanzania (BMT) na mwingine na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Akizungumza Dar es Salaam leo, Mangungu amesema usajili huo unahusisha sheria tofauti, hivyo ni muhimu kuelewa muundo wa kisheria wa taasisi hizo mbili ili kuepusha mkanganyiko kuhusu nafasi za uongozi.

“Simba Sports Club haina Mtendaji Mkuu, labda kama yupo basi ni kwenye Simba Sports Club Company ndiyo ina Mtendaji Mkuu. Kuna mmoja amesajiliwa na BMT na mwingine amesajiliwa BRELA, ni kutokana na sheria tofauti. Katiba inasema Simba Sports Club inatakiwa kuwa na Mtendaji wake na tutamtangaza kwa Taifa,” amesema Mangungu.

Kwa mujibu wa maelezo yake kuhusu katiba ya klabu hiyo, Simba Sports Club inapaswa kuwa na Mtendaji Mkuu wake, akieleza kuwa utaratibu wa kumtambua na kumtangaza kiongozi huyo unapaswa kuzingatia matakwa ya katiba.

Related Articles

Back to top button