Lusajo kuvaa kinyago kuwakabili Simba

DAR ES SALAAM:KUELEKEA dabi ya Mzizima itayopigwa keshokutwa, Kocha Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi, amesema kuwa mpango wao kuelekea mchezo huo ni tofauti na mechi walizocheza hivi karibuni.
Taoussi amesema kuwa wanaingia katika mchezo huo dhidi ya Simba wakiwa na mkakati wa kuwa na uwiano mzuri kati ya kushambulia na kujilinda. Ingawa walipoteza mchezo uliopita dhidi ya Simba, walicheza vizuri, na sasa wanakuwa makini zaidi kwa sababu tayari wanajua uimara na madhaifu ya wapinzani wao.
“Tumeandaa mpango ili tuwe makini kama tulivyokuwa kwenye mchezo dhidi ya Yanga. Tumejipanga kuhusu nini tufanye na nini tusifanye, kama ambavyo tumefanya mazoezini. Katika safu ya ulinzi lazima tuwe imara na haraka kwa sababu Simba wana mawinga wazuri na mabeki wa pembeni wanaotumia nafasi zao vizuri,” amesema Taoussi.
“Lakini pia tumefanyia kazi eneo la kumalizia na kufunga. Katika mchezo uliopita tulitengeneza nafasi nyingi, hivyo tumewaelekeza wachezaji wetu wawe makini ndani ya boksi kwa sababu mabao mengi tunayofunga hutokana na nafasi hizo. Lazima tutengeneze nafasi nyingi ili tushinde dhidi ya Simba na kulipa kisasi,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, beki wa Azam FC, Lusajo Mwaikinda, ataanza kutumia kinyago cha kinga usoni baada ya kuumia mfupa wa shavu. Kinyago hicho kitamsaidia kupona haraka na kumfanya ajisikie imara zaidi akiwa uwanjani.