Malaika Gray na Marioo kuachia ‘My Fever’ kesho

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Malaika Gray, kuachia wimbo wake wa kwanza My Fever, kesho aliomshirikisha msanii wa Bongo Fleva, Marioo.
Malaika, mwenye sauti yenye mvuto na mwonekano wa kistaa, anaingia kwenye tasnia hiyo inayotawaliwa na majina makubwa yakiwemo Zuchu na Nandy, huku ujio wake ukiibua matarajio kuhusu nafasi yake katika muziki wa Tanzania.
Wimbo huo unatarajiwa kutoka Oktoba 30, 2026, umebeba mchanganyiko wa midundo ya Afrobeats, Bongo Fleva na R&B, ukizungumzia hisia za mapenzi na mvuto kati ya watu wawili.
Malaika amesema ameamua kuanzia nyumbani Tanzania kwa kuwa anaamini muziki wake unaweza kupata nafasi kubwa zaidi duniani bila kusahau mizizi yake.
“Nilitaka kuanza nyumbani kwa sababu moyo wangu uko Tanzania na katika bara hili ninalolifahamu na kulipenda. Hata hivyo, nafanya muziki kwa ajili ya kila mtu ambaye unaweza kumfikia. Nyumbani ni mwanzo wa safari yangu, si mwisho,” amesema.
Malaika ameandika wimbo huo kwa kushirikiana na Marioo, huku Abbah Process akihusika katika utayarishaji wake.
Video ya My Fever ilirekodiwa kwa siku mbili katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, ikionyesha mandhari ya Bahari ya Hindi, masoko, daladala, saluni na maisha ya kila siku ya jiji hilo. Video hiyo imeongozwa na Joma na kumshirikisha Marioo.
Kwa upande wake Marioo amesema Malaika ana kipaji cha kweli na amefurahishwa kuwa sehemu ya kazi yake ya kwanza, huku akitarajia kufanya naye kazi nyingine katika siku zijazo.
Malaika, aliyelelewa kati ya Tanzania na Afrika Kusini, kwa sasa anasomea Vocal Performance and Music Business katika Chuo cha Muziki cha Berklee kilichopo Boston, Marekani.
Wimbo huo umetolewa kupitia Africori, kampuni iliyo chini ya Warner Music Group, na unapatikana katika majukwaa mbalimbali ya muziki ya kidijitali.
Kupitia ujio huo, Malaika ameweka wazi mwanzo wa safari yake ya muziki yenye matarajio ya kimataifa, huku akipanga kushirikiana na wasanii kutoka Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika mwaka 2027.
Ingawa bado ni mapema kutabiri nafasi yake katika ushindani wa muziki wa kike nchini, ujio wake unaongeza jina jipya la kufuatilia katika Bongo Fleva.




