Platform: Mimi na Muna Love tumebaki wazazi wa mtoto wetu

DAR ES SALAAM: Msanii wa Bongo Fleva, Platform, ameweka wazi kuhusu uhusiano wake na mama mtoto wake Muna Love, uliisha zamani kwa sasa wamebaki kuwa wazazi wa mtoto wao, Test Moon.
Platform amesema kuwa licha ya kutokuwa tena kwenye uhusiano wa kimapenzi na Muna Love, bado anamkumbuka mtoto wao na anaamini kuwa alipo akiwa na mama yake ana furaha na amani.
Akizungumza kuhusu hali ya uhusiano wao kwa sasa, Platform amesema:
“Mimi na Muna Love mahusiano yetu yaliisha kipindi cha nyuma sana, tumebaki wazazi wa mtoto wetu Test Moon. Nina imani mwanangu alipo anafuraha na amani,” amesema Platform.
Muna Love, ambaye aliwahi kujihusisha na shughuli za sanaa, ikiwemo uigizaji na muziki wa injili, kwa mujibu wa taarifa zilizopo, kwa sasa anaishi nje ya Tanzania.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa Muna amewahi kudokeza kuhusu maisha yake ya nje ya nchi kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii.
Kauli ya Platform inaweka wazi kuwa, kwa upande wake, uhusiano wa kimapenzi na Muna Love ni historia, huku jukumu lao la pamoja likiendelea kuwa malezi ya mtoto wao, Test Moon.




