RT yawapa tano wanaridha kwa mafanikio Japan

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT) limewapongeza wanariadha na viongozi wa Tanzania walioshiriki katika mbio za Nagai City Marathon nchini Japan, baada ya kufanya vizuri na kutwaa medali za dhahabu na fedha.
Katika ujumbe wake wa pongezi uliotolewa leo, RT imewapongeza wanariadha hao kwa ushindi walioupata katika mbio za kilomita 42.195 na 21, hatua inayodhihirisha uwezo wa wanariadha wa Tanzania kushindana na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Katika mbio za kilomita 42.195 kwa wanaume, Michael Kishiba alitwaa medali ya dhahabu baada ya kushika nafasi ya kwanza, huku Charles Boay akimaliza wa pili na kupata medali ya fedha. Kwa wanawake, Vaileth Kidas aliibuka mshindi na kutwaa dhahabu.
Kwa upande wa mbio za kilomita 21, Fabian Sulle alishinda kwa wanaume na kutwaa medali ya dhahabu, huku Joseph Panga akimaliza wa pili na kujipatia fedha. Katika upande wa wanawake, Agnes Protas aliibuka mshindi na kutwaa medali ya dhahabu.
Ushirikiano kati ya Nagai City Marathon na Tanzania umewezeshwa na mwanariadha mkongwe, Kanali Juma Ikangaa, kwa kushirikiana na wadau kutoka Japan, ukiwa na lengo la kukuza na kuendeleza vipaji vya riadha nchini.
Mafanikio hayo yanaongeza chachu katika juhudi za kuendeleza riadha Tanzania na kuwapa wanariadha fursa ya kushiriki mashindano ya kimataifa, kupata uzoefu na kuonesha uwezo wao katika medani za kimataifa.




