Nyumbani

Simba yaruhusiwa mashabiki dhidi ya 15 de Agosto

DAR ES SALAAM: MASHABIKI wa Simba wameruhusiwa kuingia uwanjani kushuhudia mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya 15 De Agosto ya Equatorial Guinea utakaochezwa kesho, Oktoba 21, 2026, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa Simba kufanya mazungumzo na wapinzani wao hao na kufanikiwa kuwashawishi kubadili msimamo wa awali wa kutaka mchezo huo uchezwe bila mashabiki.

Kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa leo, Simba imesema ilifanya juhudi kubwa katika mazungumzo hayo kwa kutambua umuhimu wa mashabiki katika mchezo wa soka na mchango wao kwa timu.

Awali, mchezo huo ulipangwa kuchezwa bila mashabiki kufuatia uamuzi wa upande wa 15 De Agosto, hali iliyowalazimu wapenzi wa Simba kutarajia kufuatilia pambano hilo kupitia televisheni.

Hata hivyo, kufuatia makubaliano hayo mapya, mashabiki sasa watapata fursa ya kuishuhudia timu yao moja kwa moja uwanjani, huku klabu hiyo ikiahidi kutangaza viingilio vya mchezo huo baadaye.

Katika hatua nyingine, Simba imesema mchezo huo pia utaoneshwa kupitia skrini kubwa katika maeneo ya Mwembeyanga na Mbagala Zakheim kwa ajili ya mashabiki watakaofuatilia pambano hilo nje ya uwanja.

Related Articles

Back to top button