Mariah Carey ambwaga kaka yake mahakamani

NEW YORK: MWANAMUZIKI, Mariah Carey ameshinda kesi ya kashfa iliyofunguliwa dhidi yake na kaka yake, baada ya jaji kutoa uamuzi kwa niaba yake.
Mtandao wa Billboard, umefafanua jaji alitupilia mbali kesi hiyo ya Morgan Carey, akisema kuwa hakukidhi vigezo vya kisheria vya kumshtaki dada yake.
Iko hivi, Morgan alijaribu kushtaki kuhusiana na kitabu cha Mariah cha mwaka 2020, The Meaning of Mariah Carey, akilenga sehemu za kitabu hicho zilizodokeza kuwa aliwahi kuuza dawa za kulevya na kuwa na tabia ya vurugu wakati wa utoto wao.
Imeelezwa kuwa jaji aliandika: “Mahakama inaona kuwa mdai hajatoa hoja za kutosha kuonyesha kuwa mdaiwa alikuwa na nia mbaya ya makusudi.”
Jaji aliongeza kuwa Morgan ameshindwa kuwasilisha ushahidi wowote unaoonesha kuwa Mariah alidanganya kuhusu yeye kwenye kitabu hicho.
Wakili wa Mariah, John Rosenberg, ameaiambia Billboard: “Bi. Carey anafurahishwa na ukweli kwamba mahakama imetambua kuwa kitabu chake kinagusia masuala muhimu yenye maslahi kwa umma, na imetupilia mbali madai yote ya kashfa yaliyotolewa na kaka yake.”




