Nyumbani

Tembo Queens yaanza safari ya ubingwa Afrika

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu Tanzania (TAFF) limeanza maandalizi ya timu ya taifa ya wanawake, Tembo Queens, kwa ajili ya mashindano ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu.

Akizungumza na Spotileo Dar es Salaam Ofisa Habari wa TAFF, Khalidi Msabaha, amesema kikosi hicho kimeanza maandalizi kwa kukusanya wachezaji kutoka mikoa mbalimbali nchini, hatua inayolenga kujenga timu yenye ushindani kabla ya mashindano hayo.

Amesema wachezaji hao kutoka Dar es Salaam, Songwe, Pwani na maeneo mengine walikutana kwenye Uwanja wa Uhuru kwa kambi ya awali ya wiki moja, ambako walipata mazoezi na mafunzo ya mchezo huo.

Msabaha amesema kikosi cha kwanza cha Tembo Queens kilitangazwa rasmi juzi, huku maandalizi ya hatua inayofuata yakisubiri uamuzi kuhusu ufadhili wa kambi kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Amesema shirikisho limeomba msaada huo kwa kuwa bajeti yake haitoshelezi kugharamia mahitaji yote ya kambi, hivyo wachezaji wataitwa tena kwa maandalizi zaidi baada ya kupata majibu kuhusu ombi hilo.
Msabaha amesema awali mashindano hayo yalitarajiwa kufanyika Tanzania, lakini bado hakuna taarifa rasmi iliyothibitisha kama nchi hiyo itakuwa mwenyeji au mashindano yatahamishiwa nje ya nchi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button