Infantino aomba radhi akosa majibu mpango wa kombe la dunia

ZURICH, Uswisi: RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ameomba radhi kufuatia kushindwa kwa mpango wa kuwakaribisha wawekezaji binafsi kuwekeza katika mashindano ya Kombe la Dunia, lakini amekosolewa kwa kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha kuhusu suala hilo.
Infantino alikabiliwa na maswali magumu Alhamisi katika kikao cha Baraza la FIFA kilichofanyika kwa faragha mjini Zurich, Uswisi. Mpango huo, uliojulikana kama FIFA Forward Enterprise (FFE), ulikuwa miongoni mwa masuala makuu yaliyojadiliwa.
Mpango huo ulitangazwa mwishoni mwa Julai, ukiwa na lengo la kuruhusu wawekezaji binafsi kuwekeza katika mashindano makubwa ya FIFA.
Hata hivyo, uliondolewa baada ya kukabiliwa na upinzani kutoka mashirikisho mbalimbali, yakiwemo UEFA ya Ulaya, AFC ya Asia na CONCACAF.
Rais wa Shirikisho la Soka Ujerumani, Bernd Neuendorf, ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la FIFA, alisema maswali mengi muhimu yaliulizwa katika kikao hicho, lakini hakupata majibu ya kuridhisha.
Naye Debbie Hewitt, Makamu wa Rais wa FIFA na Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka England, alimtaka Infantino kutoa nyaraka zote za mpango huo na kujibu maswali yaliyoulizwa.
Katika maelezo yake, Infantino aliomba radhi kwa mapungufu yaliyotokea katika utoaji wa taarifa na mashauriano na wadau. Hata hivyo, alisisitiza kuwa mpango huo ulikuwa pendekezo tu, si makubaliano yaliyokuwa yamekamilika, na kwamba sasa umeondolewa kabisa na hautarejeshwa kwa namna yoyote.
Infantino, aliyeiongoza FIFA tangu mwaka 2016, anatarajiwa kuwania tena urais wa shirikisho hilo Machi mwakani. Hata hivyo, mpango huo na mabishano mengine vimeibua upinzani kutoka kwa baadhi ya mashirikisho ya Ulaya, huku Hewitt akisema bado hajapata taarifa zinazoweza kubadili msimamo wake kuhusu uongozi wa Infantino.




