Featured

Lady Jaydee miaka 26 jukwaani, bado hajachoka

SWALI: Umefanya muziki kwa muda mrefu, nini kimekusaidia kudumu hadi sasa?
LADY JAYDEE: Nyakati zinabadilika. Kazi unayofanya inabidi uifanye kutokana na wakati uliopo, lakini muonekano wako unabaki kuwa uleule. Kinachobadilika ni nyakati. Kadiri umri unavyoongezeka, unaendelea kupata uzoefu na kujifunza mambo mapya.

Binadamu tumeumbwa kila siku tunatamani kutimiza jambo fulani. Kwa hiyo hata ukifanikiwa kitu kimoja, unasema nataka kitu kingine zaidi. Hakuna ile steji ambayo unafika ukasema sasa nimemaliza, mwisho wa ndoto yangu. Hapana, maisha yanaendelea.

SWALI: Muziki nao umebadilika sana tangu ulipoanza. Unafanyaje ili kuendana na mabadiliko hayo?

LADY JAYDEE: Mazingira yanabadilika, kwa hiyo na wewe unatakiwa kubadilika kutokana na wakati uliopo. Kama leo kuna jambo limetokea kwenye jamii, unaweza kuzungumzia jambo hilo. Kesho likitokea jambo jingine, nalo unaweza kulizungumzia.

Mabadiliko kwenye kazi ya sanaa yanatokana na mabadiliko katika jamii, vitu ambavyo watu wanaviona, wanakutana navyo na uzoefu wanaoupata kila siku. Huwezi kufanya sanaa bila kuangalia kinachoendelea katika jamii.

 

SWALI: Kwa nini unaamini baadhi ya nyimbo zinaweza kudumu kwa miaka mingi bila kupoteza maana?

LADY JAYDEE: Kwa sababu ni maisha ya kweli. Kila binadamu analia na kila binadamu anacheka. Kila sehemu kuna watu wa aina mbalimbali. Kuna watu wanaopendana, kuna wasio waaminifu kwenye mahusiano, kuna furaha na kuna huzuni.

Vitu vingi duniani vinafanana. Kwa hiyo unapoimba kitu ambacho ni cha ukweli kutokana na mazingira ya maisha ya kila siku, ni rahisi kitu hicho kuendelea kuwepo kwa miaka mingi.

Machozi hayana kustaafu. Watu wamekuwa wakilia tangu zamani na wataendelea kulia. Vivyo hivyo, mambo ya mapenzi, usaliti na mahusiano yamekuwepo tangu mabibi na mababu zetu. Kwa hiyo ukiimba kuhusu jambo kama hilo, mada hiyo inaweza kudumu milele.

SWALI: Baada ya miaka yote hii, bado unaona kuna kitu ambacho hujakitimiza?

LADY JAYDEE: Ndiyo. Binadamu siku zote ana hamu ya kupata kitu zaidi. Ukishafanikiwa kitu fulani, unaangalia kingine. Kwa hiyo siamini kwamba kuna sehemu unafika unasema sasa nimemaliza kila kitu.

Maisha yenyewe yanaendelea, na kila siku kuna kitu kipya cha kujifunza au kufanya.

SWALI: Utambulisho wako wa muziki umekuaje mpaka umeweza kuitunza kwa muda wote huu?

LADY JAYDEE: Nafikiri utambulisho wangu haujawahi kuhama sana kwa muda mrefu. Katika kutengeneza brand lazima uwe na kitu ambacho kinakuwa kimejengeka.

Kuna wasanii ambao ukisikia unajua huyu anaimba nyimbo za mapenzi, mwingine anaimba nyimbo za huzuni na kadhalika. Ukishajua njia ambayo watu wamekupendezea, hata ukitoka kidogo na kufanya vitu vingine, lazima uwe na njia ya kurudi kwa sababu mwisho wa siku muziki ni biashara.

Lazima ujue wateja wako wanapenda nini. Nafikiri kudumu kwangu na kusema Jay Dee yupo kwa muda mrefu kunatokana pia na mimi kudumisha kitu ambacho hakitoki nje ya Jay Dee.

SWALI: Kuna aina ya muziki ambayo bado hujafanya na ungependa kujaribu?

LADY JAYDEE: Sina neno la muziki wowote kwa sababu ninaamini muziki mzuri haujalishi umeingia kwenye aina gani. Lakini pia muziki ni kitu cha ndani sana. Unatakiwa ufanye kitu ambacho kwa wakati huo unataka kufanya na umeamua kwamba unataka kufanya hiki.

Kwa hiyo inaweza ikatokea. ‘Never say never’. Lakini kuna vitu vingine havijatokea na pengine havitatokea. Hiyo ndiyo maisha.

SWALI: Unaonaje namna jamii inavyowahukumu wanawake kutokana na mavazi yao?
LADY JAYDEE: Jamii iache kuwaangalia wanawake tofauti. Kama mwanaume anaweza kutembea akiwa amevaa kwa namna fulani na mwanamke akifanya hivyo anaonekana vibaya, hilo si sawa.

Watu wengine wanavaa kwa sababu wanapenda kuvaa hivyo, wengine kwa ajili ya kazi zao au kwa ajili ya kujieleza. Tabia ya mtu si nguo yake.

Kwa hiyo jamii isiwa hukumu sana wanawake kutokana na namna wanavyovaa. Kila kazi ina namna yake ya mavazi. Ukienda benki, kwa mfano, kuna mavazi yanayofaa kwa mazingira hayo.

Wapewe nafasi na uhuru wa kujieleza.

SWALI: Mbali na muziki, una mpango gani wa kugusa maisha ya jamii?

LADY JAYDEE: Mwaka huu tumesaini ushirikiano na kampuni nchini Marekani na tutafanya kazi kwa pamoja. Ni kitu ambacho nakiona kinaweza kuwa kizuri kwa kupata maoni kutoka kwa watu wengine na mimi kuchangia mawazo yangu.

Pia, ninapoenda mikoa mbalimbali kufanya shoo, nataka kusaidia jamii. Tarehe 11 nitakuwa Mwanza nikisaidia wanawake, mabinti na baadhi ya vijana, ingawa kipaumbele ni wanawake.

Ninaangalia wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wanaohitaji mitaji midogo kwa ajili ya kuinua sehemu ambazo wamekwama. Nilianza Arusha, Mwanza ni mkoa wa pili.

SWALI: Utahakikisha vipi msaada unawafikia watu wanaostahili?

LADY JAYDEE: Nitashirikiana na viongozi wa mtaa ambao watakuwa wanawafahamu watu hao. Watanihakikishia kwamba ni kweli wana biashara na wanahitaji msaada, si matapeli.

Tutachagua watu kadhaa, kama 10, na kuwawezesha.

SWALI: Unatarajia kufanya shoo na nani Mwanza?

LADY JAYDEE: Nitafanya shoo na mwenzangu Kidumu. Itakuwa The Bridge, Jumatano, siku ya mkesha wa Nyerere Day.

Mimi shoo zangu mara nyingi huwa na wasanii wengi sana, lakini kwenye hii ni mimi na Kidumu tu.

 

SWALI: Kuna msanii mwingine ambaye unatamani sana kufanya naye kazi?

LADY JAYDEE: Siwezi kutaja jina moja maalumu kwamba huyu ndiye napenda kufanya naye kazi. Mimi ni Jay Dee wa wote, ndiyo maana naitwa dada mkubwa.

Ukiangalia tena kuchagua kati ya wadogo zako, unaweza kuonekana kama ni ubaguzi. Kwa hiyo nafasi iko wazi kwa mtu yeyote ambaye kutakuwa na ‘chemistry’ na kama kuna kitu ambacho tutaendana, hakuna shida.

SWALI: Ruge Mutahaba alikuwa na nafasi gani katika safari yako ya muziki?

LADY JAYDEE: Ruge alifanya kazi na mimi mara ya kwanza kama meneja wangu chini ya Smooth Vibe Project. Tulisaini mkataba wa albamu mbili ambazo ni Machozi na Binti.

Tulifanya kazi vizuri na kazi zetu zilikuwa na mafanikio. Kwa hiyo mchango wake ulikuwa mkubwa katika safari yangu ya muziki.

SWALI: Baada ya zaidi ya miaka 20, unaiona vipi safari yako?

LADY JAYDEE: Nawashukuru sana watu kwa kunisapoti kwa miaka yote hii. Kama Jay Dee, safari bado inaendelea.

Muziki hauna tarehe ya kustaafu. Hakuna umri wa kustaafu kwenye kazi Hii si kazi ya kuajiriwa na mtu, ni kipaji ambacho Mungu amekupa. Kwa hiyo mpaka sauti ikate.

Related Articles

Back to top button