Muziki

De La Rose: Sijaacha muziki, nakuza ubunifu kwa AI

MAREKANI: MSANII wa muziki na mtengeneza maudhui anayeishi nchini Marekani, De Wabulassa, maarufu De La Rose, amesema hajaacha muziki kama baadhi ya watu wanavyodhani, bali amepanua wigo wa ubunifu wake kwa kutumia teknolojia ya akili mnemba (AI), inayomsaidia kutengeneza maudhui na kuwafikia mashabiki wengi zaidi.

Akizungumza na Spoti Leo, De La Rose amesema matumizi ya teknolojia hiyo ni sehemu ya mabadiliko anayoyafanya katika shughuli zake za kisanii, akitumia vipaji vyake mbalimbali kuwasilisha mawazo na kazi zake kwa njia tofauti.

Amesema yeye si mwanamuziki pekee, bali pia ni mtunzi wa nyimbo, mtayarishaji wa muziki na msanii wa sanaa za picha, hivyo anaamini uwezo wake wa ubunifu haupaswi kufungiwa katika eneo moja la sanaa.

Kwa mujibu wa msanii huyo, teknolojia ya AI imemwezesha kubadilisha hadithi, hisia na mawazo yanayochochea utengenezaji wa muziki wake kuwa picha na video zinazowapa mashabiki nafasi ya kuelewa kazi zake kwa mtazamo mpana zaidi.

Amesisitiza kuwa matumizi ya AI hayamaanishi kuondoa nafasi ya ubunifu wa binadamu, bali ni nyenzo inayowawezesha wasanii kutekeleza mawazo yao kwa urahisi na kuyawasilisha kwa namna inayovutia hadhira.

“Ujumbe, hadithi na hisia zinazopatikana katika kazi zetu za kibunifu bado vinatokana na mimi mwenyewe, huku AI ikirahisisha utengenezaji wa video ambazo kwa njia za kawaida zingehitaji gharama kubwa,” amesema De La Rose.

Ameeleza kuwa teknolojia hiyo inampa nafasi ya kuendeleza mawazo yake ya kisanii kwa kuyageuza kuwa maudhui yanayoonekana, bila kupoteza ujumbe anaotaka kuufikisha kwa mashabiki kupitia muziki wake.

Aidha, De La Rose anaona matumizi ya AI kuwa fursa muhimu kwa wasanii huru barani Afrika na katika jamii ambazo hazijapata uwakilishi mkubwa katika tasnia ya burudani ya kimataifa.

Amesema teknolojia hiyo inaweza kuwasaidia wasanii hao kuwasilisha kazi zao kwa ubunifu zaidi na kupanua wigo wa kufikia hadhira, hasa pale ambapo gharama za uzalishaji wa maudhui ya kiwango cha juu zimekuwa changamoto.

Kwa mtazamo wake, maendeleo ya teknolojia yanatoa nafasi kwa wasanii kuchunguza mbinu mpya za kujieleza na kuunganisha muziki na sanaa nyingine, huku wakibaki na udhibiti wa mawazo na ujumbe unaotokana na ubunifu wao.

De La Rose anaendelea kusisitiza kuwa mabadiliko anayoyafanya hayamaanishi kuachana na muziki, bali ni njia ya kuupanua ubunifu wake na kutumia teknolojia kama nyenzo ya kufikisha kazi zake kwa mashabiki wengi zaidi.

Related Articles

Back to top button