Marry K: Namheshimu Diamond, hata namba yake sina

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini Tanzania, Marry K, amekanusha madai yanayomhusisha kimapenzi na nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, akisema anamuheshimu msanii huyo na hana hata namba yake ya simu.
Marry K amesema ukaribu wake na Diamond unatokana na shughuli za kikazi na matukio mbalimbali ya burudani, ikiwemo sherehe, hivyo si sahihi kuhitimisha kuwa wana uhusiano wa kimapenzi kutokana na kukutana kwao mara kwa mara.
Marry K amesisitiza kuwa anamuheshimu Diamond Platnumz kutokana na nafasi yake katika tasnia ya muziki na kwamba hana sababu ya kumtongoza.
“Namuheshimu sana. Nimekutana naye kwenye kazi, labda kama hivyo kwenye kibao kata cha mwanae. Namba ya Diamond sina, wananisingizia,” amesema Marry K.
Kauli hiyo imekuja huku majina ya wasanii maarufu yakiendelea kuhusishwa na mijadala kuhusu maisha yao binafsi, hasa pale wanapoonekana pamoja katika matukio ya kijamii na shughuli za kikazi.
Hata hivyo, Marry K ameweka wazi kuwa kukutana na msanii huyo hakumaanishi kuwa kuna uhusiano wa kimapenzi baina yao, akisisitiza kuwa anachokifahamu ni heshima na ushirikiano unaotokana na kazi za burudani.
Kwa kauli hiyo, Marry K amepinga uvumi unaomhusisha na Diamond Platnumz, akiwataka wanaomzungumzia kuzingatia ukweli kuhusu ukaribu wake na mwanamuziki huyo.




