Nyumbani

Safari yasaka vipaji 22

DAR ES SALAAM: SAFARI Lager imewataka mashabiki wa soka nchini kuwa sehemu ya msako wa vipaji kwa kupendekeza wachezaji wanaoamini wana uwezo wa kufika mbali, ikiwa ni sehemu ya msimu wa tatu wa Safari Lager Cup unaolenga kupata wachezaji 22 watakaounda kikosi kimoja.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu huo jana, Mkuu wa Masoko wa Tanzania Breweries Limited (TBL), Khensani Mkhombo, amesema watu walio karibu na soka katika jamii mara nyingi ndio wanaofahamu vipaji vinavyostahili kupewa nafasi kabla havijafahamika kwa kiwango kikubwa.

“Watu walio karibu zaidi na soka mara nyingi hujua vipaji vilipo kabla ya mtu mwingine yeyote. Wanamjua mchezaji ambaye kila mtu katika jamii anaamini anastahili nafasi,” amesema Mkhombo.

Amesema kupitia mpango wa ‘Maskauti Bingwa’, mashabiki watasaidia kuwaelekeza wataalamu kwenye wachezaji wanaoamini wanastahili kuonekana, huku tathmini na uamuzi wa mwisho ukifanywa na wataalamu wa ufundi wa soka.

Msimu huo utatafuta wachezaji 22 wenye umri wa miaka 18 hadi 21 kutoka Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya, ambao watapata nafasi ya kushiriki katika Safari Lager Champions na baadaye kucheza dhidi ya Yanga Januari 30, 2027.

Jumla ya timu 80 zitasajiliwa, timu 20 kutoka kila mkoa, zikiwa na jumla ya wachezaji 880. Usajili utaanza Oktoba 6 hadi 24, kabla ya bonanza la kwanza kufanyika Oktoba 25 katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Bonanza hilo litafuatiwa na Mwanza Novemba 7, Arusha Novemba 21 na Dar es Salaam Desemba 5, ambapo maskauti watapata nafasi ya kuwatathmini wachezaji katika mazingira halisi ya ushindani.

Kwa mujibu wa waandaaji, tathmini haitazingatia mabao au matukio ya ustadi pekee, bali pia uwezo wa kiufundi, uelewa wa nafasi, ufanyaji maamuzi, utembeaji uwanjani, nidhamu, mtazamo, uwezo wa kufundishika na namna mchezaji anavyocheza chini ya presha.

Mchezaji mmoja atakayebainika katika mchakato huo pia atapata nafasi ya kufanya majaribio na Yanga, ingawa nafasi hiyo haitoi hakikisho la kupewa mkataba wa kulipwa.

Related Articles

Back to top button