Afrika Mashariki

Kocha Kenya, McCarth azihofia Morocco, Senegal

NAIROBI: Kocha wa Taifa la Kenya, Benni McCarthy, amewataka mashabiki wa Harambee Stars kuwa na matarajio ya kweli kuelekea AFCON 2027, akisema timu hiyo bado ina safari ndefu kufikia kiwango cha mataifa makubwa barani Afrika.

McCarthy amesema Kenya inahitaji muda wa kujenga kikosi imara, hasa kutokana na tofauti ya uzoefu na ubora wa wachezaji ukilinganisha na timu kama Morocco, Senegal na Afrika Kusini ambao wachezaji wao wengi wanacheza katika ligi kubwa za Ulaya.

Kauli hiyo imekuja baada ya Kenya kupata matokeo yasiyoridhisha katika dirisha la kufuzu AFCON 2027, ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Eritrea nyumbani kabla ya kupoteza 1-0 dhidi ya Guinea mjini Conakry.

McCarthy amesema matarajio ya Kenya kushinda kwa urahisi dhidi ya timu kubwa kama Afrika Kusini, Morocco na Senegal si rahisi kutokana na tofauti ya ubora wa wachezaji na uzoefu wa mashindano.

“Kama watu wanatarajia niifunge Afrika Kusini, Morocco au Senegal, ni jambo gumu sana. Ni kazi ambayo haiwezekani kutokana na wachezaji ambao nchi hizo weni wana ubora na wanacheza nje,” McCarthy amesema.

Kocha huyo pia amegusia changamoto ya kutumia wachezaji wanaocheza ndani ya Kenya, akisema ligi ya FKF Premier League ilikuwa bado haijaanza wakati wa maandalizi hayo, hivyo wachezaji hao hawakuwa wamecheza mechi za ushindani msimu huo.

“Ni rahisi kwa watu walioko nje kusema huyu ndiye kocha bora au huyu ndiye mchezaji bora, lakini unapokuwa upande huu ndipo unaona jinsi ilivyo ngumu,” amesema.

Akizungumzia mchezo wa kirafiki dhidi ya Rwanda mjini Kigali, McCarthy amesema anautumia kama kipimo muhimu cha kuona kiwango ambacho Kenya inapaswa kufikia kabla ya kukutana na timu kama Afrika Kusini.

Amesema mchezo huo pia utampa nafasi ya kuwajaribu wachezaji wapya na kuona uwezo wao, huku akisisitiza kuwa kila mchezaji anayavaa jezi ya Kenya anapaswa kutoa kiwango chake bora.

Kenya ni miongoni mwa wenyeji wa AFCON 2027 pamoja na Tanzania na Uganda, hivyo McCarthy anaamini maandalizi ya muda mrefu na uzoefu wa michezo ya kimataifa ni muhimu ili Harambee Stars iweze kushindana kwa heshima katika mashindano hayo.

Related Articles

Back to top button