Vijana Dar wajitokeza kuwania Nyota Big msimu wa pili

DAR ES SALAAM: VIJANA wenye vipaji mbalimbali wamejitokeza katika usaili wa Serengeti Lite Nyota Bigi Msimu wa Pili, uliolenga kuwapa nafasi ya kuonesha uwezo wao na kupata fursa ya kuendeleza vipaji vyao.
Usaili huo umewakutanisha vijana wenye vipaji vya kuimba, kucheza, kuigiza, kuchekesha, uanamitindo pamoja na ubunifu katika nyanja mbalimbali, huku kila mmoja akipewa nafasi ya kuonyesha uwezo wake mbele ya wataalamu wa tasnia.

Kupitia ushirikiano na KUNTA Africa, programu hiyo inalenga kuwahamasisha vijana kuamini vipaji vyao, kuviendeleza na kutumia ubunifu katika kujenga fursa zaidi kupitia kaulimbiu ya “Lite Your Imagination.”
Baada ya Dar es Salaam, usaili wa kutafuta Nyota Bigi utaendelea katika miji ya Arusha, Dodoma na Mwanza, ambako vijana wengine watapata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na kuwania nafasi ya kuwa Nyota Bigi wa msimu huu.

Safari ya kumtafuta Nyota Bigi wa Msimu wa Pili bado inaendelea, huku vijana kutoka maeneo mbalimbali wakipewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.




