Mastaa

Rick Ross akamatwa na polisi, awatuliza mashabiki

MIAMI: RAPA Rick Ross amekamatwa leo Alhamisi baada ya kwenda polisi mwenyewe kituoni kwa tuhuma za kushambulia na kumdhuru mwanamke anayeelezwa ni ‘ex-girlfriend’ wake.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya Idara ya Polisi ya Kaunti ya Miami-Dade, Mtandao wa TMZ umeripoti mwanamke huyo alitoa taarifa hiyo juzi Jumanne ingawa tukio hilo lilitokea Agosti 28, mwaka huu.

Mwanamke huyo amewafafanulia polisi kuwa siku ya tukio alikuwa amelala kwenye nyumba yao ya pamoja na Rick, ambapo rapa huyo alimwamsha na kumuuliza maswali akiwa na hasira juu ya picha ‘aliyo-tagiwa’ kwenye mtandao wa kijamii na ghafla akamvaa mwilini.

Kingine, Rick alimuuliza kwanini amekuwa akimdanganya, na kumpiga kibao kabla ya kumuuliza juu ya kuwa na uhusiano na mwanaume mwingine ambaye mara kadhaa mwanamke huyo anadai alikuwa akikataa lakini Rick hakumuelewa na kuendelea kumshambulia.

Mengine aliyowaeleza polisi ni kwamba alikabwa mno kiasi cha kuanza kuishiwa pumzi, kubamizwa ukutani na mengineyo.

Mwisho, aliwapa picha za ushahidi wa majeraha yake.

Ingawa picha walizopewa polisi hazijafahamika ni zipi lakini wiki iliyopita, mwanamke wa zamani wa Rick, Jazzma Kendrick aliweka mtandaoni, picha za majeraha yake usoni na kueleza aliyemfanyia hivyo ni mkongwe huyo.

“Siku ambayo Rick alipiga mdomo wangu, ndio siku niliyoondoka. Sifahamu vitu vingi, ila najua mwanaume anayenipiga, ni mwanaume ambaye hajawahi na hatokuja kunipenda,” Jazz alindika ujumbe huo kusindikiza picha hizo.

Mawakili wa Rick, Steve Sadow na Bradley Horenstein wameieleza TMZ kuwa rapa huyo ambaye jina lake kamili ni William Roberts II, anatuhumiwa kimakosa na mpaka sasa hawajaelewa dhumuni la mwanamke wake huyo wa zamani.

“Halafu ‘ex-girlfriend’ hakuripoti hata polisi mpaka baada ya mwezi tangu kutokea kwa tukio hilo analodai yeye. Bwana Roberts hana hatia hapa na ameshakana mashitaka yote.

“Anaomba kwa heshima kwamba marafiki zake, mashabiki na umma kwa ujumla wasihukumu hali hiyo kabla ya wakati wake, na badala yake waiache michakato ya kisheria ichukue mkondo wake,” walifafanua mawakili hao.

Rick au Rozay, 50 anatarajiwa kupanda kizimbani kwa mara ya kwanza juu ya mashtaka hayo Oktoba 22, mwaka huu.

Aidha, Rozay anatarajiwa kuwa nje kwa dhamana ya Dola 5,000 kwa kosa la kwanza na Dola 1,000 kwa kosa la pili, mashtaka ambayo kwa ujumla yanatambulika kama unyanyasaji wa nyumbani.

Related Articles

Back to top button