Muziki

Ashimba arudi na Asili Akili

DAR ES SALAAM: MWIMBAJI, mtunzi wa nyimbo na mpiga gitaa Andrew Shimba ‘Ashimba’ anatarajia kuzindua wimbo wa Asili Akili Oktoba 2, 2026, Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kuelekea kutolewa kwa albamu kamili Desemba 9, mwaka huu.

Kazi hiyo imejengwa katika mizizi ya utamaduni wa Tanzania, ikichanganya sauti za Kinyamwezi, Kisukuma na Kiswahili na mitindo ya Afropop na muziki wa Afrika Mashariki.

Asili Akili inatafakari utambulisho, maisha ya jamii na uwezo wa mwanadamu wa kufikiri, kuelewa na kutofautisha mema na mabaya, huku Ashimba akitumia muziki kusimulia maisha ya Mtanzania wa sasa.

Katika kazi hiyo, msanii huyo amegusa pia masuala ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo umaskini, rushwa, ukosefu wa usawa na changamoto za vijana, huku akisisitiza amani, utu, maendeleo na ajira.

Akizungumza na Spotileo Ashimba amesema Albamu hiyo ina nyimbo 14, zikiwemo Kuzaliwa, Mali ya Umma, Utajiri, Risiti, Mtoto, Afrika, Asili Akili, Mjasiriamali, Kiapo, Utekaji Dunia na Pesa Chafu.

“Uzinduzi utafanyika Oktoba 2 utakuwa sehemu ya maonesho maalum kuelekea kutoa albamu kamili Desemba 9, 2026,nitafanya maonesho mengine Arusha na Nairobi, ambayo tarehe zake zitatangazwa baadaye,”amesema Ashimb ana kuwaomba mashabiki na wadau kumuunga mkono siku hiyo.

Ashimba, mwenye asili ya Tabora kupitia Nkinga na Sikonge, amekuwa akijenga muziki wake katika usimulizi wa hadithi na utambulisho wa kitamaduni, huku akitumia gitaa na ala mbalimbali kuunda sauti inayotofautisha kazi zake.

Asili Akili itakuwa albamu ya tatu ya Ashimba baada ya Nuru Nyikani ya mwaka 2009 na Wakukaya iliyotolewa mwaka 2013.

Related Articles

Back to top button