Burudani

Bhushan Kumar atajwa tajiti mkubwa Bollywood

MUMBAI: MTAYARISHAJI wa filamu nchini India, Bhushan Kumar, ametajwa kuwa mmoja wa watu wenye utajiri mkubwa zaidi katika sekta ya Bollywood, huku utajiri wake ukikadiriwa kufikia takribani Shilingi trilioni 10 za Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya Hurun India Rich List 2026 iliyoripotiwa na Hindustan Times Septemba 29, 2026, Bhushan Kumar, ambaye ni mkuu wa kampuni ya muziki na burudani ya T-Series, ana utajiri unaokadiriwa kufikia ₹36,300 crore, sawa na takribani TSh trilioni 10.0.

Utajiri huo unatokana zaidi na shughuli zake katika sekta ya muziki, filamu na uzalishaji wa maudhui kupitia T-Series, badala ya kuwa mwigizaji au muongozaji wa filamu.

Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa Bhushan Kumar amekuwa mtu pekee kutoka sekta ya burudani aliyeingia katika orodha 100 ya matajiri nchini India kwa mujibu wa orodha hiyo ya mwaka 2026. Amewekwa katika nafasi ya 87.

Kwa upande mwingine, orodha hiyo inaonesha kuwa Shah Rukh Khan anakadiriwa kuwa na utajiri wa takribani ₹10,000 crore, ambao ni sawa na takribani TSh trilioni 2.75 kwa kiwango cha ubadilishaji fedha cha Septemba 29, 2026.

Taarifa hizi zinaonesha ukubwa wa biashara iliyo nyuma ya tasnia ya Bollywood, ambako mapato makubwa hayatokani na uigizaji pekee, bali pia muziki, uzalishaji wa filamu, haki za maudhui na biashara nyingine zinazohusiana na burudani.

Related Articles

Back to top button