Burudani

Jaydee alamba dili Universal Music Group

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI mkongwe kutoka Tanzania, Judith Mbibo maarufu Lady Jaydee, anayejulikana pia kama ‘Queen of Bongo Fleva’ amesaini mkataba wa usambazaji kupitia kampuni ya muziki ya Universal Music Group East Africa (UMG EA).

Dili hilo linaenda sambamba na Lady Jaydee kusherehekea miaka 25 kwenye tasnia ya muziki wake na kuwa nguzo ya muziki katika eneo hilo.

Lady Jaydee aliyezaliwa mwaka 1979, safari ya muziki wake ilianza miaka ya 1990 ambapo alianza kama rap ana baadae akaibukia katika uimbaji wenye mafanikio makubwa uliomzolea mashabiki wakutosha nchini Tanzania, Kenya na nchi zingine za Ukanda wa Afrika Mashariki.

Akiwa na albamu 9 za studio na zaidi ya tuzo thelathini za ndani na nje ya nchi, Lady Jaydee amekuwa mwanamapinduzi katika kuboresha muziki wa Bongo Fleva kupitia kuachia muziki wake hadi sasa, kuzunguka na kufanya maonyesho mbalimbali nchini Tanzania, barani Afrika na duniani kote, kwa kuangalia vipindi halisi vya TV kama vile The Voice of Africa’.

Kwa kuongezeka kwa wasanii katika orodha ya vipaji Afrika Mashariki, UMG EA imetoa fursa ya kuleta mwanga mpya katika ukanda huu na kusafirisha vipaji katika safu za kimataifa.

Lady Jaydee aingia kwenye orodha ya wasanii wa UMG tayari kuchagiza tasnia hiyo zaidi.

Universal Music Group (UMG) ni kampuni inayoongoza ulimwenguni katika kuleta burudani ya muziki, ikiwa na safu pana ya biashara zinazojishughulisha na muziki uliorekodiwa, uchapishaji wa muziki, uuzaji na maudhui ya sauti inayoendeshwa ndani ya zaidi ya nchi 60 duniani.

Related Articles

Back to top button