Miss World kutangaza Utamaduni wamakabila mbalimbali Tanzania

DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema itahakikisha walimbwende watakaoshiriki shindano la miss world mwakani kila mmoja atachagua kabila atakalo litangaza kwenye jukwaa hilo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mashindano hayo, akieleza kuwa washiriki wa miss world kutoka mataifa mbalimbali watapewa nafasi ya kuchagua kabila la Tanzania na kujifunza utamaduni wake.
Amesema mshiriki atakayechagua kabila fulani atapata fursa ya kufahamu mambo mbalimbali yanayohusiana na jamii hiyo na baadaye kuiwakilisha kwenye jukwaa la kimataifa wakati wa mashindano.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hiyo inalenga kutumia uwepo wa washiriki kutoka mataifa mbalimbali kutangaza utamaduni wa Tanzania kwa watu wanaofuatilia mashindano hayo duniani.
Amesema Tanzania ina makabila mengi yenye tamaduni tofauti na Serikali imeona umuhimu wa kutumia mashindano hayo kuyaweka katika jukwaa la kimataifa ili dunia ifahamu zaidi utamaduni wa Watanzania.
“Wengine wanaweza kuwa Wajerumani, Waitaliano, Wakuwaiti au Wachina, wakachagua kabila la Watengwa, Wasukuma au Wamasai na kujifunza utamaduni wao,” amesema.
Amesema utekelezaji wa mpango huo utafanyika kwa kushirikiana na kamati ya maandalizi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha jamii zinazohusika zinapata nafasi ya kushiriki katika kuonesha utamaduni wao.
Ameongeza kuwa mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali ikiwamo Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha, hatua ambayo amesema itasaidia kusambaza fursa zinazotokana na ujio wa wageni katika maeneo hayo.




