Ligi Kuu

JKT Tanzania yasuka upya safu zake

DAR ES SALAAM: KOCHA Msaidizi wa JKT Tanzania, George Mkete, amesema timu hiyo inatumia mapumziko ya kalenda ya FIFA kuimarisha safu zake zote, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate utakaochezwa Oktoba 9, mwaka huu, mkoani Arusha.

Akizungumza na Dailynews Digital kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo Dar es Salaam leo amesema kuwa benchi la ufundi limeweka mkazo katika kuboresha safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji ili kuongeza ushindani wa kikosi hicho kinacholenga kumaliza Ligi Kuu katika nafasi nne za juu

Amesema matokeo ya michezo sita iliyopita hayajawa mazuri kwa matarajio yao, baada ya kushinda miwili, kupoteza mitatu na kutoka sare moja.

“Kwa ujumla huo si mwanzo mzuri kwa timu ambayo inalenga kumaliza katika nafasi nne za juu, tunatumia kipindi hiki kurekebisha mapungufu yetu turudi tukiwa imara,” amesema.

Amesema kwa sasa hawana mpango wa kuweka kambi nje ya Dar es Salaam, badala yake wataendelea na maandalizi yao jijini humo.

Mkete amesema wachezaji wanaendelea na mazoezi na kurejea majumbani, huku timu ikitarajia kurejea kambini kati ya Septemba 25 na 26.

Pamoja na hayo, wamepanga kucheza mchezo wa kirafiki kati ya timu kutoka Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza.

Kuhusu hali za wachezaji, amesema kikosi kinaendelea vizuri kiafya, isipokuwa majeraha ya kawaida ambayo hayajaleta changamoto kubwa.

Related Articles

Back to top button