Nyumbani

Msuva atoa wito kwa mashabiki kuiunga mkoni Stars kuelekea AFCON 2027

DAR ES SALAAM:MSHAMBULIAJI mkongwe wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Simon Msuva, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu hiyo katika kipindi hiki muhimu cha kampeni ya kufuzu fainali za AFCON 2027.

Msuva ametoa wito huo wakati Taifa Stars ikiendelea na kambi yake ya maandalizi katika Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam, chini ya Kocha Mkuu Miguel Ángel Gamondi. Kambi hiyo ilianza rasmi Septemba 19, 2026, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya timu kuelekea michezo yake ya kimataifa.

Akizungumzia umuhimu wa sapoti kutoka kwa mashabiki, Msuva amesema mafanikio ya Taifa Stars hayawezi kupatikana kwa wachezaji pekee uwanjani, bali yanahitaji pia nguvu na hamasa kutoka kwa mashabiki walio nje ya uwanja.

Amesema Watanzania wanapaswa kujitokeza kwa wingi na kujaza viwanja ili kuipa timu hamasa zaidi wakati inapokuwa ikipambana katika michezo yake ya kimataifa.

Msuva amesisitiza umuhimu wa mashabiki kuiunga mkono Taifa Stars, hasa katika kipindi ambacho Tanzania ipo katika maandalizi kuelekea fainali za AFCON 2027, ambazo Tanzania ni mmoja wa wenyeji pamoja na Kenya na Uganda.

Taifa Stars inatarajiwa kuanza kampeni zake za Septemba kwa mchezo dhidi ya Guinea-Bissau, utakaochezwa Septemba 25, 2026, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kuanzia saa 10:00 jioni.

Baada ya mchezo huo, Taifa Stars itakutana na Madagascar Septemba 29, 2026, katika mchezo utakaochezwa Casablanca, Morocco, ambapo Madagascar imechagua Morocco kuwa mwenyeji wa mchezo huo.

Awali, Taifa Stars ilitarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Ghana Oktoba 4, 2026, lakini mchezo huo umevunjika baada ya Ghana kupanga kucheza dhidi ya Morocco. Kutokana na hali hiyo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea kutafuta wapinzani wengine wawili kwa ajili ya michezo ya kirafiki.

Related Articles

Back to top button