Muziki

Jux: Ndoa imenipa ubunifu kwenye uandishi

MAREKANI: MSANII wa Bongo Fleva, Juma Mkambala ‘Jux’, amesema kuingia katika ndoa na Priscilla Ojo kumempa uzoefu na mwanga zaidi katika uandishi wa nyimbo zake zinazohusu mapenzi.

Jux amesema maisha ya ndoa yamemsaidia kuelewa zaidi hisia na uzoefu wa kimapenzi, jambo ambalo limemrahisishia kuandika nyimbo pamoja na kuchagua maneno yanayoendana na ujumbe anaotaka kuwafikishia mashabiki wake.

Amesema tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuingia katika ndoa, kwa sasa anapata urahisi zaidi anapoandika nyimbo za mapenzi kutokana na uzoefu anaoupata katika maisha yake ya kila siku.

Kwa mujibu wa Jux, ndoa hiyo pia imekuwa sehemu ya safari yake ya kimuziki, ikimpa mtazamo mpana zaidi katika namna anavyowasilisha hisia kupitia muziki.

Mbali na maisha ya ndoa, Jux anaendelea kupanua wigo wa muziki wake nje ya Afrika Mashariki, ambapo kazi zake zimeanza kufuatiliwa na mashabiki kutoka maeneo mbalimbali barani Afrika, ikiwemo Afrika Magharibi.

Priscilla Ojo anatokea Nigeria, jambo ambalo pia limeongeza ukaribu wa Jux na hadhira ya Afrika Magharibi kupitia muziki na shughuli zake mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Jux ametangaza kufanya ziara nchini Marekani, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza shughuli zake za muziki na kukutana na mashabiki wake waliopo nchini humo.

Ziara hiyo inatarajiwa kuwa sehemu ya juhudi zake za kuendelea kujenga hadhira ya kimataifa na kuitangaza zaidi kazi yake ya muziki nje ya Afrika Mashariki.

Related Articles

Back to top button