Tamasha la kuombea Uchaguzi Mkuu kufanyika mikoa 26

DAR ES SALAAM:TAMASHA la kuombea Uchaguzi Mkuu linatarajiwa kufanyika katika mikoa 26 ya Tanzania, likianza jijini Dar es Salaam mwaka huu.
Tamasha hilo litapambwa na waimbaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, likiwa na lengo la kuhimiza amani na mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Machi 24, 2025, Mkurugenzi wa Msama Promotion, Alex Msama, amesema ibada hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Lengo ni kuweka umoja na ushirikiano miongoni mwa Watanzania, kuwaombea viongozi watakaochaguliwa ili waweze kutuongoza kwa hekima na busara,” alisema Msama.
Tamasha hilo litashirikisha waimbaji kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, na Rwanda, ambao wanatarajiwa kutoa burudani na kushiriki maombi maalum kwa ajili ya uchaguzi.
Aidha, Msama amewaomba viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha wanatumia lugha zenye heshima katika mikutano yao ya kampeni badala ya lugha za matusi, ili kuhimiza siasa safi na yenye maadili kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Pia, amewataka wadau na watu mbalimbali kujitokeza kutoa ushirikiano wa kudhamini tamasha hilo ili kuhakikisha linafanikiwa na kuleta ujumbe wa amani na mshikamano kwa Watanzania wote