Muziki

Linah: Sitachanganya tena mapenzi na kazi

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Linah Sanga, amesema amejifunza kutokana na changamoto alizowahi kukutana nazo baada ya kuchanganya kazi na mahusiano ya kimapenzi, hivyo hataki kurudia kosa hilo katika safari yake ya muziki.

Linah amesema awali alikuwa akichanganya masuala ya kazi na mahusiano yake binafsi, jambo ambalo baadaye lilimletea changamoto katika kazi zake za muziki na kumfanya atambue umuhimu wa kuweka mipaka kati ya maeneo hayo mawili.

Akizungumzia hatua yake ya kuanza kusimamiwa kikazi na lebo ya African Princess, inayomilikiwa na msanii Nandy, Linah amesema alipata ushauri muhimu kuhusu namna ya kutenganisha maisha yake binafsi na kazi.

Kwa mujibu wa Linah, Nandy alimshauri kuweka nguvu na umakini zaidi katika muziki wake na kuhakikisha mahusiano ya kimapenzi hayaathiri majukumu yake ya kikazi.

Amesema, kwa mfano, anapokuwa na majukumu ya kwenda studio, anatakiwa kuheshimu muda uliopangwa na kufika kwa wakati, badala ya kutoa visingizio vinavyohusiana na masuala ya kimapenzi.

“Nimepewa ushauri mzuri wa kutenganisha kazi na mapenzi. Kama nina kazi ya studio, ni lazima niheshimu muda wa kazi na kutimiza majukumu yangu,” amesema Linah.

Hata hivyo, Linah amefafanua kuwa makubaliano yake ya kikazi na African Princess hayamzuii kuwa katika mahusiano ya kimapenzi, bali anapaswa kuhakikisha maisha yake binafsi hayaingilii majukumu na malengo yake ya muziki.

Amesema amepokea ushauri huo kwa mtazamo chanya na amedhamiria kuutumia katika kujenga nidhamu na umakini zaidi katika safari yake ya muziki.

Related Articles

Back to top button