Oprah Winfrey kufanya show Las Vegas

LAS VEGAS: Mwanahabari, mtangazaji na mfanyabiashara maarufu wa Marekani, Oprah Winfrey, anajiandaa kuingia katika hatua nyingine kubwa ya kazi yake ya burudani kupitia onesho jipya la moja kwa moja litakalofanyika katika ukumbi maarufu wa Sphere, Las Vegas nchini Marekani.
Onesho hilo, linalotajwa kwa jina la “Oprah Winfrey’s AHA,” linatarajiwa kuwa la kipekee kutokana na mchanganyiko wa maudhui ya Oprah na teknolojia ya kisasa inayopatikana katika ukumbi huo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kuhusu mradi huo, onesho hilo litakuwa na muda wa takribani saa mbili, likimpa Oprah nafasi ya kuwasiliana moja kwa moja na mashabiki wake katika mazingira tofauti na yale waliyozoea kumuona kwenye vipindi vya televisheni.
Sphere ni miongoni mwa kumbi zinazovutia zaidi kwa sasa katika ulimwengu wa burudani kutokana na matumizi yake ya teknolojia kubwa za picha na sauti.
Jina “AHA” pia limeongeza hamu miongoni mwa mashabiki, hasa kwa kuwa Oprah amejenga kwa muda mrefu taswira inayohusisha mazungumzo yenye kugusa maisha, uzoefu binafsi, mafanikio na mabadiliko ya mtu.
Taarifa kuhusu onesho hilo zimeanza kuzua gumzo katika sekta ya burudani, huku mashabiki wakisubiri kuona namna Oprah atakavyolitumia jukwaa kubwa la Sphere kuleta utofauti na vipindi vyake vya kawaida.
Kwa jina kubwa kama Oprah Winfrey, onesho hilo linatarajiwa kuvutia hisia kutoka kwa mashabiki wake ndani na nje ya Marekani. Umaarufu wake wa kimataifa unaweza kufanya mradi huo kuwa miongoni mwa matukio yanayofuatiliwa kwa karibu katika kalenda ya burudani ya Las Vegas “Oprah Winfrey’s AHA”.




