Mkuu wa Kamati ya Olimpiki za Majira ya Baridi 2030 ajiuzulu

PARIS, Ufaransa: Edgar Grospiron, mkuu wa kamati inayosimamia maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya mwaka 2030 nchini Ufaransa, amejiuzulu baada ya miezi kadhaa ya mvutano ndani ya kamati hiyo.
Kujiuzulu kwa Grospiron ni pigo jingine kwa maandalizi ya michezo hiyo, baada ya viongozi kadhaa wa juu kuondoka katika kamati ya maandalizi katika kipindi cha hivi karibuni. Hali hiyo imeibua maswali kuhusu uongozi na namna maandalizi ya Olimpiki yatakavyoendelea.
Kamati ya maandalizi, inayojulikana kama COJOP, ilisema kuondoka kwa Grospiron ni sehemu ya mabadiliko yaliyopangwa katika uongozi.
Kamati hiyo ilisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda maslahi ya mradi na kuhakikisha maandalizi yanaingia katika hatua mpya ya utekelezaji bila kuchelewa.
Grospiron mwenyewe alithibitisha kuondoka kwake kupitia ukurasa wake wa LinkedIn, akisema uamuzi huo umefikiwa baada ya miezi kadhaa ya mvutano ndani ya kamati.
Alisema baada ya kutathmini hali hiyo, amefikia hitimisho kwamba mazingira yaliyopo hayamruhusu kuendelea na safari hiyo.
Kujiuzulu kwake kunakuja wakati wadau muhimu wa Michezo hiyo wakiwa tayari wameonesha kutoridhishwa na uongozi wake. Serikali ya Ufaransa, pamoja na mikoa ya Provence-Alpes-Côte d’Azur na Auvergne-Rhône-Alpes, ni miongoni mwa taasisi zilizohusika katika kutoa msimamo huo.
Aidha, Kamati za Olimpiki na Paralimpiki za Ufaransa zilimweleza Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) mwezi uliopita kwamba hazikuwa tena na imani kuwa zinaweza kuendelea kufanya kazi na Grospiron. Hatua hiyo iliongeza presha dhidi ya kiongozi huyo kabla ya hatimaye kuamua kujiuzulu.
Grospiron si mgeni katika historia ya Olimpiki, kwani aliwahi kushinda medali ya dhahabu katika mchezo wa moguls wa kuteleza kwenye theluji katika Michezo ya Olimpiki ya Albertville mwaka 1992. Uzoefu huo ulimpa nafasi muhimu katika kusimamia maandalizi ya Olimpiki za 2030, lakini mvutano wa ndani ukawa changamoto kubwa katika uongozi wake.
maandalizi ya Olimpiki za Majira ya Baridi za 2030. Pamoja na kuondoka kwa Grospiron, kamati hiyo imesisitiza kuwa mchakato wa maandalizi utaendelea, huku ikilenga kuingia katika awamu mpya ya uendeshaji na utawala wenye utulivu zaidi.




