
DAR ES SALAAM: MWANAMITINDO na Mkurugenzi wa Kidoti Foundation, Jokate Mwegelo ‘Kidoti’, ametoa mchango wa Sh milioni 10, huku mtoto wake Phiona akitoa Sh milioni 5 kwa niaba ya wazazi wake, katika hafla ya KMK Executive Gala iliyofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mchango huo umefikia jumla ya Sh milioni 20, ikiwa ni sehemu ya tukio lililoandaliwa katika kuadhimisha miaka 10 ya “Neema Inayomiminika.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Jokate amewataka Wakatoliki kumtolea Mungu kwa hali na mali, akisisitiza kuwa utoaji wa kweli hautegemei utajiri wa mtu bali moyo wa mtu katika kumshukuru Mungu.
Jokate amesema hakuna haja ya mtu kusubiri kuwa tajiri ili aweze kumtolea Mungu, bali kila mmoja anapaswa kutoa kulingana na kile alichobarikiwa nacho.
“Kutoa ni moyo, siyo utajiri. Ukimnyima Mungu, naye atakunyima; ukimtolea, utaona baraka zake,” amesema Jokate.
Amesema kuwa imani na moyo wa kutoa ni miongoni mwa mambo muhimu yanayomfanya mtu kutambua na kuthamini baraka anazopokea katika maisha yake.
Hafla hiyo ya Kwaya ya Mtakatifu Kizito Executive Gala, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, imewakutanisha waumini na wadau mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea miaka 10 ya neema pamoja na kuendelea kuhamasisha moyo wa utoaji na kumshukuru Mungu.
Katika halfa hiyo wamefanikiwa kukusanya jumla ya kiasi cha zaidi ya Sh Milioni 200 za kitanzania.



