Cuthbert avuna matunda ya kiwango bora

DODOMA: KIWANGO bora alichoonesha Denis Cuthbert katika mchezo wa Polisi Tanzania dhidi ya Dodoma Jiji kimemzawadia tuzo ya Mchezaji Bora wa mchezo, hatua anayoiangalia kama motisha ya kuendelea kufanya vizuri zaidi.
Cuthbert alikuwa sehemu ya kikosi cha Polisi Tanzania kilichopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji jana huku akionesha uwezo uliomfanya kutwaa tuzo hiyo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Cuthbert amesema tuzo hiyo ni jambo kubwa kwake na amemshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na wazazi wake kwa kuendelea kumuombea na kumtia moyo katika safari yake ya soka.
“Leo nimepata tuzo ya mchezaji bora wa mechi, ni kitu kikubwa katika maisha yangu. Nawashukuru wazazi wangu ambao wanaendelea kuniombea. Namshukuru Mwenyezi Mungu na naahidi kufanya zaidi na zaidi,” amesema Cuthbert.
Kwa ushindi huo Polisi Tanzania iko katika nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi saba baada ya kushinda jumla ya michezo miwili na kupata sare Moja.




