Africa

Broos amuonya Mosimane kuifundisha Bafana Bafana

JOHANNESBURG: Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Hugo Broos, amempa tahadhari Pitso Mosimane kuhusu changamoto kubwa inayoweza kumkabili iwapo atarejea kuinoa Bafana Bafana.

Broos, mwenye umri wa miaka 74, amemtaja Mosimane kama mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, huku akifichua misingi iliyomsaidia kupata mafanikio wakati wa kuinoa timu hiyo na namna alivyokabiliana na shinikizo kutoka nje ya uwanja.

Hata hivyo, raia huyo wa Ubelgiji amekiri kuwa bado anaikosa sana soka na angependa kuendelea kushiriki katika mchezo huo kupitia nafasi nyingine tofauti na ukocha.

Broos anaamini kurejea kwa Mosimane kwenye kikosi cha taifa kunaweza kuja na changamoto kubwa, hasa katika kukabiliana na ushawishi wa wenye klabu na mawakala wa wachezaji.

Akizungumza na Nieuwsblad, Broos alisema Mosimane atahitaji kuwa imara katika kufanya maamuzi ya kikosi bila kuathiriwa na watu wenye maslahi nje ya timu.

Alisema Broos. “Unajua, Afrika Kusini bado haina kocha. Tegemeo ni Pitso Mosimane, kocha aliyefanikiwa kutoka Afrika Kusini.”

Broos aliongeza kuwa Mosimane anaweza kujikuta katika mazingira ambayo yamewahi kuwepo miaka kadhaa iliyopita, ambapo viongozi wa klabu na mawakala walikuwa wakijaribu kuathiri uteuzi wa wachezaji wa timu ya taifa.

“Wanajua kwamba akija, itakuwa kama kurudi miaka mitano nyuma. Wamiliki wa klabu na mawakala watakuwa wakimpigia simu kocha ili kushawishi uteuzi wa timu,” alisema.

“Niliwafukuza Wote”

Broos alifichua kuwa wakati akiwa kocha wa Bafana Bafana hakuruhusu mawakala au wenye ushawishi nje ya timu kuingilia maamuzi yake ya uteuzi.

“Niliwafukuza wote. Kama mmoja alipiga simu, nilimwambia moja kwa moja: ‘Sizungumzi na mawakala,’” alisema.

Kwa Mosimane, iwapo atateuliwa kuwa kocha wa Bafana Bafana, uwezo wa kudhibiti shinikizo kutoka kwa wenye klabu na mawakala unaweza kuwa moja ya mitihani yake mikubwa katika kuhakikisha anaunda timu kwa misingi ya uwezo wa wachezaji na mahitaji ya timu ya taifa.

Related Articles

Back to top button