CAF yafungua zabuni za haki za matangazo Afcon 2027

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF)) limefungua rasmi mchakato wa zabuni kwa ajili ya kupata kampuni na vyombo vya habari vitakavyonunua haki za matangazo ya AFCON 2027, mashindano yatakayofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda.
Taarifa hiyo imechapishwa leo Jumatatu, Agosti 24, 2026, na Broadcast Media Africa, huku CAF ikithibitisha pia kupitia tovuti yake rasmi kuwa imezindua ‘Invitation to Tender (ITT)’ kwa haki za matangazo ya Afcon pamoja 2027.
Zabuni hiyo inahusisha haki za matangazo ya ‘Free-to-Air’ (FTA) na ‘Pay-TV’ katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. CAF imeweka pia lugha mbalimbali zitakazohusika katika kifurushi hicho, ikiwemo Kiswahili, Kiingereza, Kireno, isiZulu, Wolof, Yoruba na lugha nyingine za eneo husika.
Kwa mujibu wa CAF, kampuni na vyombo vya habari vinavyotaka kushiriki katika mchakato huo vinatakiwa kuwasilisha zabuni zao kabla ya Septemba 14, 2026 saa 17:00 kwa muda wa Cairo. Hata hivyo, haki za Pay-TV kwa lugha ya Kifaransa hazijajumuishwa katika zabuni ya AFCON 2027.
Afcon Pamoja 2027 inatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania, Kenya na Uganda kuandaa kwa pamoja michuano mikubwa ya timu za taifa ya Afrika. Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa tukio kubwa la michezo kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa Tanzania, habari hii ni muhimu kwa TV, redio, majukwaa ya kidijitali na kampuni za habari, kwa sababu inafungua rasmi mchakato wa ushindani wa kupata haki za kuonesha michuano hiyo. CAF pia imesema zabuni hiyo inalenga kuhakikisha mashabiki wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wanapata matangazo ya mashindano hayo kupitia lugha mbalimbali.




