Motsepe ataja dawa ya Caf kuepuka mgogoro Afcon 2027

CAIRO, Misri: Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amesema shirikisho hilo limeanza kufanya mageuzi makubwa ili kuhakikisha Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 halikumbwi na sintofahamu iliyozuka katika fainali ya mwaka 2025.
Motsepe alisema CAF imejifunza kutokana na tukio hilo lenye utata na tayari imepitisha kanuni mpya pamoja na kuimarisha usimamizi wa waamuzi na teknolojia ya Video Assistant Referee (VAR), ili kulinda uadilifu wa mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Fainali ya AFCON 2025 kati ya Senegal na wenyeji Morocco iligeuka gumzo baada ya wachezaji wa Senegal kutoka uwanjani dakika za mwisho wakipinga uamuzi wa mwamuzi. Nahodha Sadio Mané aliwashawishi wenzake kurejea uwanjani baada ya kusimama kwa dakika 17, na Senegal ikaibuka na ushindi wa mabao 1-0 baada ya muda wa nyongeza.
Hata hivyo, miezi kadhaa baadaye CAF ilibatilisha matokeo hayo na kuipa Morocco ushindi wa mabao 3-0 kwa kile ilichokitaja kuwa Senegal ilikiuka kanuni kwa kusitisha mchezo. Uamuzi huo uliivua Senegal ubingwa wa Afrika na kuzua hasira kubwa nchini humo.
Shirikisho la Soka la Senegal lilipinga uamuzi huo na kuwasilisha rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), huku likitoa tuhuma za upendeleo dhidi ya CAF.
Akizungumzia sakata hilo, Motsepe alisema suala hilo sasa lipo mikononi mwa CAS na CAF itaheshimu uamuzi wowote utakaoamuliwa na mahakama hiyo.
“Mchakato uko CAS na uamuzi wowote watakaoufanya tutauheshimu na kuutekeleza. Migogoro ya maamuzi ya waamuzi haipo Afrika pekee, hata Kombe la Dunia limewahi kushuhudia maamuzi yaliyobishaniwa,” alisema Motsepe.
Alifafanua pia kuwa kauli yake ya awali kuhusu kuchoshwa na maswali yanayohusu fainali hiyo ilitafsiriwa vibaya, akisema hakumaanisha kuwa amechoshwa na wanahabari, bali alikusudia kueleza kuwa mjadala huo mrefu umekuwa wa kuchosha kwa wadau wote wakati kesi ikiwa bado haijapatiwa uamuzi.
Kuelekea AFCON 2027, Motsepe alisema CAF imeweka mkazo katika kuimarisha mafunzo kwa waamuzi, waendeshaji wa VAR na makamishna wa mechi ili kuhakikisha sheria za mchezo zinaeleweka na kutekelezwa kwa usawa katika kila mchezo.
Alisisitiza kuwa lengo kuu la CAF ni kuhakikisha mashabiki, wachezaji na mataifa yanayoshiriki yana imani kuwa ushindi utapatikana kwa uwezo wa timu uwanjani, badala ya maamuzi yenye utata kutoka kwa waamuzi au VAR.
“Tumejifunza kutokana na yaliyotokea Morocco na tayari tumepitisha sheria zitakazozuia tukio kama hilo kujirudia. Tunataka kila mtu aamini kuwa timu inashinda kwa sababu ndiyo ilikuwa bora, si kwa sababu ya maamuzi yenye utata ya mwamuzi au VAR,” alisema Motsepe.
Kauli ya rais huyo wa CAF imekuja wakati maandalizi ya AFCON 2027 yakiendelea, huku shirikisho hilo likiahidi kufanya kila linalowezekana kurejesha imani ya wadau na kuhakikisha mashindano hayo yanaendeshwa kwa uwazi, haki na uadilifu.




