Luizer Mbutu hofu ya Mungu ndio siri ya mafanikio yangu

MSANII wa muziki wa dansi nchini, Luizer Nyoni Mbutu, amesema kuwa siri kubwa iliyomsaidia kuendesha maisha yake kwa mafanikio ni kuwa na hofu ya Mungu pamoja na kuongozwa na mafundisho ya Roho Mtakatifu katika kila hatua ya maisha yake.
Akizungumza na Spoti LEO, Lwiza amesema kuwa vijana na jamii kwa ujumla wanapaswa kujifunza kutafuta maendeleo yao kwa njia halali badala ya kutegemea mali au mafanikio ya watu wengine.
Amesema tabia ya kutamani vitu vya wengine imekuwa chanzo cha kuporomoka kwa maadili katika jamii, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na kuwa na subira katika kutafuta mafanikio.
“Kinachoniongoza katika maisha ni hofu ya Mungu na kumsikiliza Roho Mtakatifu. Pia watu wanapaswa kujifunza kutafuta vyao na kuacha kutegemea mali za wenzao, jambo ambalo litasaidia kujenga nidhamu na maadili mema,” amesema Luizer.
Msanii huyo ameongeza kuwa kizazi cha sasa kinapaswa kuelewa kuwa mafanikio ya kweli yanahitaji muda, uvumilivu na kufuata taratibu sahihi, badala ya kutaka kufikia malengo kwa njia za mkato.
Amesisitiza kuwa mtoto au kijana anatakiwa kujiepusha na tamaa na kujenga utamaduni wa kutafuta vitu vyake kwa njia halali na kwa hatua zinazostahili, kwani hakuna mafanikio yanayopatikana kwa urahisi.
“Watu wengi wanataka mafanikio ya haraka, lakini ukweli ni kwamba kila hatua ya maisha ina mchakato wake. Hakuna maisha rahisi, kila mafanikio yana gharama ya juhudi, nidhamu na uvumilivu,” ameeleza.
Luizer pia alitoa wito kwa jamii kuacha kuiga maisha ya hali ya juu ambayo hayalingani na uwezo wao wa kifedha, akisema tabia hiyo mara nyingi huwasukuma baadhi ya watu kuingia katika vitendo visivyofaa ili kuonekana wanaishi maisha ya kifahari.
Kwa mujibu Luizer wa msanii huyo, kuridhika na hatua ya maisha aliyofikia mtu na kufanya kazi kwa bidii ndiyo njia bora ya kujenga maisha yenye heshima, amani na mafanikio ya kudumu.




