Africa

Kocha mpya wa Senegal, Patrick Viera atangaza kushinda Afcon 2027

DAKAR: Nahodha wa zamani wa Arsenal na gwiji wa soka la Ufaransa, Patrick Vieira, baada ya kuteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Senegal, akipewa jukumu la kuiongoza nchi yake ya kuzaliwa ametangaza lengo lake kuu la kwanza ni kushinda taji la AFCON 2027.

Vieira mwenye umri wa miaka 50, aliyezaliwa jijini Dakar kabla ya kuhamia Ufaransa akiwa na umri wa miaka minane anachukua nafasi ya Pape Thiaw, ambaye aliondolewa kwenye nafasi hiyo kufuatia Senegal kutolewa katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026.

Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) limesema uteuzi wa Vieira unaendana na mpango wake wa kuimarisha benchi la ufundi na kufikia malengo makubwa ya taifa hilo katika soka.

Vieira anakabidhiwa timu ya Senegal ikiwa imetoka katika kipindi cha mvutano.
Kocha aliyemtangulia, Pape Thiaw, alijikuta kwenye mvutano mkubwa wakati wa fainali ya AFCON 2025 baada ya kuiongoza timu yake kuondoka uwanjani kupinga penati iliyotolewa Morocco katika muda wa nyongeza.

Sasa Vieira ana jukumu la kuijenga upya Senegal na kuiandaa kwa mashindano yajayo, huku AFCON 2027 ikiwa moja ya malengo makubwa ya timu hiyo.

Miongoni mwa changamoto za kwanza za Vieira zitakuwa katika mechi za kufuzu michuano ya kufuzu AFCON 2027 mechi hizo zinatarajiwa kuanza kupigwa kuanza mwezi ujao.

Vieira anaingia Senegal akiwa na uzoefu mkubwa wa soka kutokana na historia yake ya kucheza na kufundisha. Akiwa Arsenal, alishinda mataji matatu ya Premier League na FA Cup mara nne.

Pia aliwahi kucheza na kushinda mataji akiwa na AC Milan, Inter Milan na Manchester City kabla ya kustaafu soka mwaka 2011.

Baada ya kustaafu, Vieira alianza kazi ya ukocha mwaka 2016 akiwa na New York City FC, kabla ya baadaye kufundisha Nice, Crystal Palace, Strasbourg na Genoa.

Akiwa Crystal Palace, aliiongoza klabu hiyo kumaliza nafasi ya 12 katika Premier League na kufika nusu fainali ya FA Cup msimu wa 2021/22

Related Articles

Back to top button