Africa

YANGA, SINGIDA, KMKM: Wenyewe ni wa kimataifa zaidi

MECHI za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika zinaendelea wiki hii kwa
michezo ya mkondo wa pili wakati Yanga leo watakuwa mwenyeji wa Asas Ali Sabieh ya Djibouti, Singida na KMKM zitakuwa ugenini dhidi ya JKU na St George.

Mechi za mkondo wa pili zina umuhimu mkubwa kwa kila mmoja kutafuta nafasi ya kufuzu
raundi ya kwanza ili kupigania nafasi ya kuingia hatua ya makundi.

YANGA vs ASAS
Kwa kuanza na mchezo wa Yanga utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, wataingia dimbani wakiwa na faida ya kuongoza mabao 2-0 waliyopata katika mchezo wa kwanza.

Mchezo wa kwanza ulichezwa kwenye uwanja huo, Asas ikiwa mwenyeji hivyo bado Yanga ana faida lakini hatakiwi kubweteka kwa sababu wapinzani wao sio wabaya sana huenda wakarudi kivingine.

Kinachohitajika kwa Yanga ni kuingia kwa kuwaheshimu wapinzani wao kwa kuwa Asas ilileta changamoto kidogo kwa kuonesha soka zuri ingawa walionesha udhaifu katika kufunga.

Lakini wana hatari kwa kuwa kuna muda walikuwa wanaingia kwenye eneo la Yanga kama
timu hiyo ingekuwa makini katika mchezo wa kwanza, basi wangeweza kupata mabao lakini walionekana kukosa umakini.

Pengine kocha wa Asas kuna kitu alikiona hivyo anaweza kuja akiwa amejiandaa, akiwa na
matumaini kuwa anaweza kupata mabao kama watajiandaa vizuri kwa kurekebisha madhaifu yao ya awali.

Asas ni timu inayocheza kwa tahadhari kubwa ikijilinda lakini kuna muda walikuwa wakipata mpira wanakimbia mbele. Ni timu yenye wachezaji wengi vijana na wazuri na bado wanaweza kufanya lolote na wakaishangaza Yanga.

Kwa upande wa Yanga wanaweza kuwa wanapewa nafasi kwa sababu ya utangulizi wa
mabao mawili, lakini wasijisahau na kujiona wamemaliza wanahitaji kuingia kwa tahadhari kubwa, kwa kuendelea kuwaheshimu wapinzani wao na kupata matokeo mazuri.

Yanga inaweza na imeonesha ubora tangu kuanza kwa michuano ya Ngao ya Jamii namna ilivyo na kikosi cha vijana wengi wenye uwezo na wametoka pia kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC na kushinda mabao 5-0.

Ushindi huo unaonesha dhahiri namna gani wanatoa onyo kwa wapinzani wao na zaidi
wako tayari kwa mapambano. Hicho walichokianzisha kinaleta matumaini kwa mashabiki zao na wadau wa soka wataamini kuwa wanaweza kuwakilisha vizuri.

Yanga yenye uzoefu na michuano hiyo ya kimataifa ikipata matokeo ya sare yoyote au
ushindi wowote inakwenda hatua inayofuata. Hata ikifungwa bao moja bado inakwenda.

SABABU ZA KUSHINDA
Yanga ina kila sababu ya kuondoka na mabao kibao kutokana na ubora wa kikosi chao kikiongozwa na Aziz Ki ambaye ameonesha kiwango bora, wachezaji kama Mudathir Yahaya, Pacome Zouzoua, Khalid Aucho, Hafiz Konkon, Djigui Diara na wengine hakika
wanaweza kufanya kitu kwa ajili ya furaha za mashabiki wao.

Mshindi wa mechi hiyo atakutana na mshindi wa mechi kati ya Otoho ya Congo au El Mereikh ya Sudan, ambao katika mchezo wao wa kwanza walitoka sare ya kufungana bao 1-1.

JKU vs SINGIDA
Timu hizi zitarudiana kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi. Katika mchezo wa kwanza JKU ya Zanzibar ilikula kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Singida Big Stars kwenye uwanja huo.

Leo mwenyeji ni JKU je, baada ya kupoteza mchezo wa kwanza atakuja vipi? Bila shaka unaweza kuwa mchezo mgumu kwa sababu wataingia wakiamini wana nafasi ya kupindua meza.

Ingawa Singida hawatakiwi kubweteka bali kuendelea kujipanga na kuwaheshimu wapinzani ikiwezekana kuendeleza matokeo mazuri na kuvuka hatua inayofuata.

Singida wameonesha kuwa wana wachezaji wazuri wanaopambana na wanapewa nafasi
kubwa ya kuendeleza kile ambacho wamekianzisha. Wametoka kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons waliosuluhu kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Liti
mkoani Singida.

Tayari wamerejea na wana morali ya hali ya juu, wanataka kudhihirisha ubora wao kwamba
msimu huu hawataki kubahatisha wanataka kuwa miongoni mwa timu bora za Tanzania zitakazofanya vizuri zaidi na malengo yao walisema awali ni kuingia hatua ya makundi.

Hayo yote yanaweza kutimizwa na timu kuendelea kupata matokeo mazuri. Ukiachana na
mchezo huo, mwingine ni KMKM ya Zanzibar itakuwa ugenini nchini Ethiopia kuvaana na St
George.

KMKM ilianza kampeni zake vibaya katika mchezo wa kwanza uliochezwa Azam Complex,
walipoteza mabao 2-1. Leo wataku- wa ugenini wataweza kupindua meza? Bila shaka
unaweza kuwa mchezo mgumu kwao lakini lolote linawezekana kulingana na maandalizi yao.

Tayari wamewasoma wapinzani wao, wameona madhaifu yao kama wataingia kwa tahadhari kubwa wanaweza kufanya vizuri.

Ila St George ni miongoni mwa timu za ukanda wa Afrika Mashariki zinazojitahidi na zenye uzoefu mkubwa wana nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwa kutumia uwanja wa nyumbani kwao wakiamini watakuwa mbele ya mashabiki zao.

Lakini haipaswi kuogopa na KMKM inachohitaji ni kufanya kile walichojiandaa nacho na kufanya yale ambayo wengi hawatarajii. Waoneshe ukubwa wao ili kuwapa furaha mashabiki wa soka Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Related Articles

Back to top button