Coastal Union yaapa kuisimamisha Yanga

TANGA: KOCHA wa Coastal Union, Fikiri Elias, amesema timu yake imefanya maandalizi makubwa kuelekea mchezo dhidi ya Yanga, huku akieleza kuwa wameitazama kwa kina timu hiyo kupitia michezo yake ya hivi karibuni.
Akizungumzia mchezo huo utakaochezwa Alhamis ya wiki hii, Elias amesema: “Tumejiandaa vizuri, muda wote tumekuwa kwenye maandalizi kwa ajili ya michezo yao. Tumeweza kuifuatilia Yanga kupitia michezo yake, ikiwemo dhidi ya Namungo, hivyo tumepata nafasi ya kujua namna wanavyocheza na kuweka nguvu katika kuwaandaa wachezaji wetu,”
Kwa upande wake, mshambuliaji wa Coastal Union, Farid Mussa, ambaye aliwahi kuitumikia Yanga, amesema wanatambua ubora wa wapinzani wao, lakini wamejiandaa kupambana ili kupata matokeo.
“Tunaona Yanga kwa sasa wako zuri, hasa baada ya kufanya vizuri kwenye Ngao ya Jamii. Ni timu yenye wachezaji wengi wenye uzoefu, lakini sisi kama Coastal tumejiandaa vizuri. Mchezo wetu wa kwanza tulipoteza kwa mabao, jambo ambalo halikuwa katika malengo yetu,” amesema Farid.
Farid amewataka mashabiki wa Coastal Union kuendelea kuishikilia timu hiyo, akiahidi kuwa wataingia uwanjani kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha wanapata matokeo.
“Nawaomba wana-Coastal tushikamane kwa sababu hii ni timu yetu. Katika mchezo dhidi ya Yanga tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, tunaamini tutafanikiwa,” amesema.




