Gamondi: Kipa Ken Gold ni mali
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amemsifu kipa wa Ken Gold, Castor Muhagama kwa kiwango alichoonesha timu hizo mbili zilipokutana Septemba 25 Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kocha huyo amesema golikipa huyo alipunguza idadi ya mabao ambayo wangeweza kushinda katika mchezo huo.
Amesema walitengeneza nafasi nyingi katika mchezo laikini Muhagama alifanya kazi nzuri na kuokoa mipira ya hatari mingi iliyomfikia.
“Tulitawala mpira, kwa uzoefu wa wachezaji wangu tulifanikiwa kupata alama tatu, wachezaji wamepambana kwa sababu Ken Gold walicheza kwa nguvu ,”amesema Gamondi.
Kocha huyo amesema Muhagama amefanya kazi nzuri kwa kusaidia timu yake kuokoa mipira mingi ambayo ililenga lango lake na kuonyesha ukomavu wa hali ya juu.
Ameongeza kuwa licha ya kupoteza nafasi nyingi za wazi anawapongeza wachezaji wake kwa kufanikiwa kuvuna pointi tatu.