Mbeya City, Geita Gold kuanza vita ya Ligi Kuu

MBEYA:KOCHA wa Geita Gold, Zuberi Katwila amesema kikosi chake kimejiandaa vyema na kiko tayari kwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Leo kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Akizungumzia mchezo huo, Katwila amesema wamefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo na wachezaji wanauelewa umuhimu wa kuingia uwanjani wakiwa tayari kwa ushindani.
Amesema maandalizi hayo yamewapa utayari wa kujibu kila changamoto watakayokutana nayo kutoka kwa Mbeya City, akiamini wachezaji wake watatekeleza kile walichokifanyia kazi katika mazoezi.
“Maandalizi tuliyoyafanya yametupa utayari wa kujibu kila changamoto tutakayoulizwa na mpinzani wetu,” amesema Katwila.
Kwa upande wa mchezaji wa Geita Gold, Yusuph Mhilu amesema kikosi kimejiandaa vizuri na kinatambua mchezo huo utakuwa wa ugenini, hivyo wachezaji wamejiandaa kukabiliana na mazingira ya kucheza mbele ya wenyeji.
Hata hivyo, Mbeya City nayo imeweka wazi kuwa haitarajii kupata mchezo mwepesi, huku kocha wake, Salim Mayanga akisema anatambua Geita Gold itatoa ushindani mkubwa.
“Tunatambua mchezo utakuwa mgumu na wenye ushindani, lakini maandalizi tuliyofanya yametujenga vizuri na kuwawezesha wachezaji kuelewana zaidi ndani ya uwanja,” amesema Mayanga.
Mchezaji wa Mbeya City, Hassan Dilunga amesema kikosi kimejiandaa vyema na wachezaji wako tayari kupambana kwa pamoja katika kutafuta matokeo mazuri.
Wamekutana mara Saba na kati ya hizo, Mbeya City imeshinda mara nne, imetoka sare mara tatu na huku Geita ikishinda mara Moja.
Michezo mingine itakayochezwa Leo ni Dodoma Jiji dhidi ya Pamba Jiji huku Singida ikicheza dhidi ya Fountain Gate.




