Kangwanda: Debi imenipa morali ya kuanza Yanga

DAR ES SALAAM:MSHAMBULIAJI wa Yanga, Albert Kangwanda, amesema kufunga bao la ushindi dhidi ya Simba katika mchezo wake wa kwanza wa debi kumempa morali kubwa ya kuanza safari yake mpya ndani ya klabu hiyo.
Kangwanda alifunga bao la ushindi kwa kichwa baada ya kumalizia krosi ya Chadrack Boka, katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa jana, akisema alifurahia zaidi kwa sababu bao hilo liliisaidia timu yake kupata ushindi katika mechi kubwa.
“Nimefurahi sana. Nilijua kabla ya mchezo kwamba hautakuwa rahisi. Kufunga katika debi na katika mazingira kama haya kunanipa moyo mkubwa na ninatazamia kufanya vizuri zaidi katika michezo inayofuata,” amesema Kangwanda.
Akizungumzia bao lake, Kangwanda amesema alitumia maelekezo ya kocha ya kushambulia lango kila mpira unapowekwa kutoka pembeni, jambo lililomsaidia kuwa katika nafasi sahihi wakati Boka alipopiga krosi.
“Kocha amekuwa akituambia sisi wachezaji wa pembeni kwamba tunapaswa kushambulia mpira na lango. Kila mpira unapokuwa pembeni, unatakiwa kushambulia lango. Kwa bahati nzuri mpira ulinikuta na nilichotakiwa kufanya ni hatua,” alisema.
Ushindi huo umeweka mwanzo mzuri kwa Kangwanda katika maisha yake mapya Yanga, huku akitarajiwa kuendelea na jukumu la kusaidia safu ya ushambuliaji katika michezo ijayo.
Mwisho




