Trey Songz kutua Dar kesho

DAR ES SALAAM: MWIMBAJI maarufu wa Marekani, Trey Songz, anatarajiwa kuwasili Tanzania kesho, Agosti 12, tayari kwa kutumbuiza katika tamasha la IMBEJU Sauti Moja Concert, litakalofanyika Agosti 14 katika viwanja vya TTCL Grounds, Kijitonyama, Dar es Salaam.
Ujio wa Trey Songz unatarajiwa kuwa kivutio kikubwa katika tamasha hilo litakalowakutanisha wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania, likiwa sehemu ya matukio yanayoandaliwa na CRDB Foundation kwa lengo la kuunganisha burudani na shughuli za kijamii.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema Trey Songz ndiye msanii mkubwa wa kimataifa anayetarajiwa kutumbuiza katika tamasha hilo.
“Tutakuwa na wasanii wengi ambao watatumbuiza katika tamasha hilo, japo msanii mkubwa ni Trey Songz kutoka Marekani. Hii ni sehemu ya wikiendi inayounganisha michezo, muziki na uwekezaji katika jamii,” amesema Mwambapa.
Mbali na Trey Songz, tamasha hilo litashirikisha wasanii wengine wakubwa kutoka Afrika, akiwemo BNXN (Buju) wa Nigeria na Kabza De Small wa Afrika Kusini, huku Tanzania ikiwakilishwa na Mbwaba Kilungi ‘Mbosso’ na George Mdemu ‘GNako’.
Trey Songz, ambaye amejijengea jina kubwa katika muziki wa R&B, soul na hip-hop, anafahamika kupitia nyimbo zake zilizofanya vizuri duniani kama Bottoms Up, Slow Motion, Say Aah, Na Na, Can’t Help but Wait na Heart Attack.
Ujio wake unatarajiwa kuongeza msisimko kwa mashabiki wa muziki nchini, hasa wale wanaofuatilia muziki wa R&B na wasanii wakubwa wa kimataifa.
Tamasha hilo litakuwa moja ya matukio makubwa ya burudani jijini Dar es Salaam wikiendi hiyo, likitarajiwa kuwakutanisha mashabiki wa muziki pamoja na wasanii wa ndani na nje ya Tanzania.




