Mkwasa ahimiza mkakati maalumu AFCON 2027

DAR ES SALAAM: KOCHA wa zamani wa Taifa Stars, Charles Mkwasa, amesema Tanzania inapaswa kuanza maandalizi ya muda mrefu kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa kuweka mkakati maalumu utakaowezesha kupata kikosi chenye ushindani, ikiwemo kuwatafuta wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza nje ya nchi.
Akizungumza na SpotiLeo Mkwasa amesema Tanzania, ambayo itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo pamoja na Kenya na Uganda, haiwezi kutegemea maandalizi ya muda mfupi kama inataka kushindana na mataifa makubwa ya Afrika.
Amesema jambo la kwanza ni kuwa na mpango mkakati utakaobainisha namna ya kupata wachezaji bora, maandalizi yao na programu za kuwaongezea ushindani kabla ya michuano hiyo.
“Lazima tuwe na mipango mikakati. Tuanze sasa kuandaa timu, tuangalie wachezaji tutakaowatumia na mazingira yatakayowawezesha kushindana na mataifa mengine,” amesema.
Mkwasa amesema pamoja na kuendelea kukuza vipaji vya ndani, Tanzania inapaswa kufungua milango kwa wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza katika ligi za nje, akisema uzoefu wao unaweza kuongeza nguvu ya Taifa Stars.
Ametolea mfano mataifa kama Comoro na Madagascar ambayo yamepiga hatua kwa kutumia wachezaji wa nje wanaocheza katika ligi zenye ushindani mkubwa.
“Tunapaswa kuwaangalia pia Watanzania walioko nje ya nchi. Wapo wengi wanaocheza katika mazingira ya ushindani na wanaweza kuongeza ubora wa timu yetu,” amesema.
Amesema uteuzi wa wachezaji unapaswa kuzingatia uwezo na kiwango walichonacho badala ya kuangalia wanatoka klabu gani, akisisitiza kuwa ushindani wa nafasi ndani ya kikosi ndiyo utakaosaidia kupata timu bora.
Mkwasa ameongeza kuwa mataifa mengi yaliyofanikiwa barani Afrika yana wachezaji wengi wanaocheza ligi za juu duniani, jambo ambalo limeongeza kiwango cha timu zao za taifa.



