Nyumbani

Tuzo za TFF kufanyika Desemba au Januari

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeeleza kuwa limepanga kurejesha utaratibu wa kufanya tuzo za mwisho wa msimu katika kipindi maalumu cha Desemba au Januari, badala ya kuacha muda mrefu kupita baada ya msimu kumalizika.

Rais wa TFF, Wallace Karia amesema leo kuwa tuzo hizo zitatolewa kwa washindi wa ligi na makundi mbalimbali ya wachezaji na wadau waliofanya vizuri katika msimu uliopita, huku shirikisho likianza mazungumzo na wadhamini wanaoweza kuwezesha hafla hiyo.

Amesema TFF inataka tuzo hizo ziwe sehemu ya utaratibu wa kudumu, sawa na ilivyo kwa tuzo za kimataifa zinazotolewa baada ya msimu kukamilika.

“Tutazifanya, itakuwa Desemba au Januari. Tunazungumza na wadhamini ili tuweze kufanya,” amesema Karia.

Amesema tuzo hizo zitahusisha washindi mbalimbali wa ligi, ikiwemo mabingwa na wafungaji bora, huku TFF ikiwa na mpango mpana zaidi wa kutambua mafanikio ya soka nchini.

Amesema TFF iliwahi kukumbana na changamoto katika utekelezaji wa tuzo hizo, lakini sasa imeamua kupanga mapema na kuweka mfumo utakaotumika kwa kila msimu.

Karia amesema tofauti na majukumu ya bodi zinazosimamia mashindano, TFF ndiyo yenye jukumu la kuandaa tuzo zake za kitaifa, hivyo utaratibu huo utawekwa ndani ya mipango ya shirikisho.

Related Articles

Back to top button