Africa

Twiga Stars yahamishia vita Burkina Faso

RABAT: MKUU wa msafara wa Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Somoe Ng’itu amesema kikosi hicho kimeufunga ukurasa wa mchezo wa kwanza wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 na sasa kimeelekeza nguvu zote katika maandalizi ya mchezo wa pili dhidi ya Burkina Faso.

Akizungumza nchini Morocco Ng’itu amesema benchi la ufundi linaendelea kufanya uchambuzi wa kina wa wapinzani hao kwa kutumia mbinu zilizotumika kuisoma Afrika Kusini, huku likifanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo uliopita ili kuhakikisha Twiga Stars inaingia uwanjani ikiwa katika kiwango bora.

Amebainisha kuwa mchezo dhidi ya Burkina Faso hautakuwa rahisi kwani wapinzani wao pia wanahitaji kufufua matumaini yao baada ya kupoteza mechi ya kwanza, hivyo kila upande utaingia uwanjani ukiwa na shauku ya kupata matokeo chanya.

“Huu ni mchezo mwingine wa fainali kwetu. Tunahitaji ushindi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele, wakati wao wanahitaji kurekebisha makosa yao. Tanzania inatutegemea na tupo hapa kuipa heshima nchi yetu,” amesema Ng’itu.

Twiga Stars ipo Kundi B la WAFCON 2026 pamoja na Afrika Kusini, Burkina Faso na Ivory Coast. Kila timu itacheza mechi tatu za hatua ya makundi huku timu zitakazomaliza katika nafasi za juu zikifuzu hatua ya robo fainali.

Twiga Stars inatarajiwa kuvaana na Burkina Faso Julai 31, 2026 katika mchezo unaotajwa kuwa wa muhimu kwa pande zote mbili, huku matokeo yake yakitarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuamua hatima ya timu hizo kwenye mbio za kufuzu hatua ya mtoano.

Related Articles

Back to top button