Baada ya Pep, Guardiola kuikataa Italia, Conte, Mancini na Pirlo watajwa

ROME: Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) linaendelea na mchakato wa kutafuta kocha mpya wa timu ya taifa, huku Antonio Conte, Roberto Mancini na Andrea Pirlo wakitajwa kuwa wagombea wakuu wa nafasi hiyo baada ya makocha wenye majina makubwa Carlo Ancelotti na Pep Guardiola kukataa kuifundisha timu hiyo.
Ripoti kutoka Italia zinaeleza kuwa FIGC ilifanya mazungumzo na Ancelotti, lakini kocha huyo aliamua kuendelea na majukumu yake ya kuinoa timu ya taifa ya Brazil. Baada ya hapo, Guardiola naye alihusishwa na nafasi hiyo, lakini hakukubali kuiongoza Italia kutokana na sababu zake binafsi za maslai.
Kutokana na hali hiyo, viongozi wa soka nchini Italia sasa wameelekeza macho yao kwa makocha watatu wenye uzoefu mkubwa nchini Itali.
Antonio Conte anaonekana kuwa mmoja wa wagombea wenye nafasi kubwa kutokana na rekodi yake ya mafanikio akiwa ameinoa Italia pamoja na vilabu vikubwa barani Ulaya. Nidhamu yake ya hali ya juu na uwezo wa kujenga timu zenye ushindani vinatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazomfanya kupewa nafasi kubwa.
Mwaingine anayetajwa ni Roberto Mancini, ambaye aliiongoza Italia kutwaa ubingwa wa Euro 2020, pia ametajwa kuwa anaweza kurejea kuinoa timu hiyo kutokana na uzoefu wake mkubwa na mafanikio aliyowahi kuyapata akiwa na Azzurri.
Kwa upande mwingine, Andrea Pirlo, ambaye ni kiungo wa zamani wa Italia na aliyewahi kuinoa Juventus, ameibuka kama chaguo jingine la FIGC huku akitajwa kuwa sehemu ya kizazi kipya cha makocha kinachoweza kupewa jukumu la kuijenga upya timu ya taifa.
Hadi sasa, FIGC haijatangaza rasmi kocha mpya wa Italia, lakini Conte, Mancini na Pirlo wameendelea kuongoza orodha ya makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya kuinoa timu hiyo kuelekea mashindano yajayo ya kimataifa.




