Simba yampoteza Kajuna, kuzikwa leo jioni

DAR ES SALAAM: Klabu ya Simba imepata pigo baada ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo, Iddi Kajuna, kufariki dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Simba, Kajuna aliteuliwa kushika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano mwaka jana na aliendelea kuitumikia hadi alipofariki dunia.
Kazi yake ya mwisho ilikuwa kusimamia maandalizi ya Fainali ya Kombe la CRDB iliyochezwa Julai 4, mwaka huu, visiwani Pemba.
Mbali na nafasi hiyo, Kajuna alikuwa Mjumbe wa Baraza la Ushauri lililoundwa na Rais wa Simba, Mohammed Dewji. Pia, aliwahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali ndani ya klabu hiyo, ikiwemo Kaimu Makamu Mwenyekiti mwaka 2017 na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji kuanzia mwaka 2014 hadi 2018.
Aidha, mwaka 2018 alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Mpito ya Wakurugenzi wakati Simba ilipokuwa ikifanya mabadiliko ya mfumo wa uongozi.
Uongozi wa Simba umesema mwili wa marehemu utaswaliwa leo katika Msikiti wa Maamur, Upanga, kabla ya kuzikwa katika Makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam, saa 10 alasiri.




