Mkunda: JKT msiache vipaji vya wanamichezo vipotee

DAR ES SALAAM: MKUU wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, amevitaka vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), hususan Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kuhakikisha vinatambua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo ili visiendelee kupotea, akisema hatua hiyo itawezesha kupata wachezaji bora wa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kijeshi ya Afrika na dunia.
Jenerali Mkunda amesema hayo leo alipofunga Mashindano ya Kombe la Mkuu wa Majeshi (CDF Cup) yaliyofanyika katika viwanja vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, ambapo Kamandi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliibuka mshindi wa jumla baada ya kufanya vizuri katika michezo mbalimbali.
Katika fainali ya soka iliyochezwa mapema leo, JKT iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Makao Makuu ya Jeshi na kutwaa taji hilo, huku pia ikifanya vizuri katika michezo mingine ikiwemo netiboli kwa wanawake na pool table kwa wanaume.

“Nawaasa viongozi wa timu mbalimbali, hasa JKT, msiache vipaji vikaenda kupotea. Hakikisheni mnaviendeleza ili viweze kuliletea Jeshi na Taifa mafanikio makubwa zaidi,” amesema Jenerali Mkunda.
Amesema zawadi walizopata washindi ni matokeo ya ubora, mikakati na jasho walilomwaga katika mashindano hayo, hivyo zinapaswa kuwa chachu ya kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.
“Waliofanikiwa kupata vikombe nawapongeza, na ambao hawakufanikiwa kupata tuzo wasikate tamaa. Hilo liwe chachu ya kujiandaa vizuri zaidi kwa mashindano yajayo,” amesema.

Jenerali Mkunda amesema mashindano hayo yamedhihirisha dhamira ya JWTZ ya kuendelea kukuza sekta ya michezo na kuandaa wanamichezo watakaoiwakilisha Jeshi katika mashindano ya CISM ngazi ya Afrika na dunia.
Amewataka wanajeshi watakaopata nafasi ya kuiwakilisha JWTZ kimataifa kujiandaa kwa bidii, kuzingatia nidhamu binafsi, kufuata maelekezo ya walimu na kuwa na dhamira ya kwenda kushindana na kushinda badala ya kushiriki.
Pia ametoa wito wa kuendelea kuimarisha programu za kutambua na kukuza vipaji vya michezo ndani ya vikosi vya jeshi ili kuongeza ushindani na mafanikio katika mashindano ya kimataifa.




