Morocco kuendelea na kocha Ouahbi licha ya kutupwa nje kombe la dunia

MAREKANI: Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) limethibitisha kuendelea kumuamini kocha Mohamed Ouahbi licha ya timu hiyo kutolewa katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia 2026, likisema ataendelea kuinoa timu kuelekea Kombe la Dunia la mwaka 2030 ambalo Morocco itakuwa mwenyeji mwenza pamoja na Hispania na Ureno.
Ouahbi, mwenye umri wa miaka 49, alichukua mikoba ya kuinoa Morocco mwezi Machi mwaka huu akirithi nafasi ya Walid Regragui, aliyefanikiwa kuipeleka timu hiyo katika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022 na baadaye kufika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Wakati wa kutambulishwa, Ouahbi alisema mkataba wake utaendelea hadi mwaka 2030.
Katika Kombe la Dunia 2026, Morocco ilionyesha ushindani mkubwa kabla ya safari yake kusimama katika robo fainali baada ya kufungwa mabao 2-0 na Ufaransa, matokeo yaliyomaliza ndoto za Atlas Lions kutinga hatua ya nusu fainali kwa mara nyingine.
Licha ya kuondolewa, Shirikisho la Soka la Morocco limetoa tamko likieleza kuwa lina imani kamili na Ouahbi na linaamini ndiye mtu sahihi wa kuendelea kuijenga timu kwa ajili ya mafanikio ya baadaye, hususan kuelekea Kombe la Dunia 2030 litakalofanyika kwa ushirikiano wa Morocco, Hispania na Ureno.
Ouahbi anatajwa kuwa mmoja wa makocha wenye uwezo mkubwa wa kukuza vipaji nchini Morocco, baada ya kuiongoza timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia la vijana mwaka 2025, mafanikio yaliyomsaidia kupandishwa kuinoa timu ya wakubwa.
Kwa kupewa tena dhamana hiyo, Ouahbi sasa anakabiliwa na jukumu la kuijenga Morocco kuwa moja ya timu zitakazowania mafanikio makubwa mbele ya mashabiki wake katika Kombe la Dunia 2030, huku matarajio ya taifa hilo yakiwa makubwa kufuatia mafanikio yake ya miaka ya hivi karibuni kwenye soka la kimataifa.




