Messi, Lamine Yamal: Kutoka Beseni la kuogea hadi fainali ya Kombe la Dunia

MAREKANI: WAKATI dunia ikisubiri kwa hamu fainali ya Kombe la Dunia 2026 kati ya Argentina na Hispania, picha ya mwaka 2007 inayomuonesha Lionel Messi akimuogesha mtoto mchanga Lamine Yamal imeibuka tena na kuzua gumzo kubwa mitandaoni.
Picha hiyo imegeuka kuwa moja ya simulizi zinazogusa hisia za mashabiki wa soka, ikionesha jinsi hatima ilivyowaunganisha mastaa hao wawili kwa njia isiyotarajiwa.
Picha hiyo ilipigwa mwezi Desemba mwaka 2007 wakati Messi, ambaye wakati huo alikuwa nyota anayechipukia wa Barcelona, aliposhiriki kampeni ya hisani ya kalenda iliyoandaliwa kwa kushirikiana na shirika la UNICEF.
Katika tukio hilo, Messi alimuogesha Lamine Yamal aliyekuwa na umri wa miezi mitano pekee, bila yeyote kujua kuwa mtoto huyo angekuja kuwa mmoja wa vipaji vikubwa zaidi vya soka duniani. Miaka 19 baadaye, simulizi hiyo imechukua sura mpya.
Messi, nahodha wa Argentina na bingwa mtetezi wa Kombe la Dunia, sasa anakutana na Lamine Yamal ambaye ni tegemeo kubwa la Hispania katika pambano la kuwania taji la dunia. Kutoka kuwa mtoto aliyebebwa mikononi mwa Messi hadi kuwa mpinzani wake katika mechi kubwa zaidi ya soka, Yamal ameandika historia ya kipekee inayovutia mashabiki duniani.
Kuibuka tena kwa picha hiyo kumewafanya mashabiki wengi kuelezea tukio hilo kama moja ya hadithi za kushangaza zaidi katika historia ya mchezo wa soka. Wengi wameitaja kuwa ishara ya mzunguko wa maisha, ambapo mtoto aliyewahi kuonekana mikononi mwa shujaa wake sasa anasimama uwanjani akiwa na nafasi ya kuzuia ndoto ya Messi kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo.
Fainali hiyo sasa haisubiriwi kwa sababu ya ubora wa timu pekee, bali pia kwa simulizi hii ya kipekee ambayo imeongeza uzito na mvuto wa pambano hilo.




