England yamvunja moyo Kane

ATLANTA: Nahodha wa England, Harry Kane, amesema ameumia sana baada ya timu yake kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Argentina katika nusu fainali ya Kombe la Dunia, akieleza kuwa walijaribu kulinda ushindi baada ya kupata bao la kuongoza lakini mbinu hiyo haikutosha.
England ilitangulia mbele kupitia bao la Anthony Gordon dakika ya 55, kabla ya Argentina kusawazisha kupitia Enzo Fernandez na Lautaro Martinez kufunga bao la ushindi katika dakika za nyongeza na kuipeleka timu hiyo fainali.
Akizungumza baada ya mchezo, Kane amesema England ilicheza vizuri kwa sehemu kubwa ya mechi, lakini baada ya kupata bao walijikuta wakijilinda zaidi badala ya kutafuta bao la pili.
“Baada ya kuongoza 1-0 tulionekana kujaribu kulinda matokeo. Katika kiwango hiki haitoshi. Tumeumia sana kwa sababu tumefanya kazi kubwa kufika hapa na kila mchezaji alitoa kila alichokuwa nacho,” amesema Kane.
Aliongeza kuwa Argentina iliongeza presha kubwa baada ya kufungwa, huku England ikilazimika kujilinda dhidi ya mashambulizi ya mfululizo, lakini hatimaye walishindwa kuhimili kasi hiyo.
Kane amesema licha ya kuondolewa, England imeonesha kiwango kizuri katika mashindano hayo na sasa inahitaji tu kupata kitu cha ziada katika hatua za mwisho za mashindano makubwa ili kufikia ndoto ya kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1966.




