Judo yatakiwa kuleta dhahabu Jumuiya ya Madola

DAR ES SALAAM: Serikali imewataka wachezaji wa timu ya taifa ya judo kupambana kwa nguvu zote katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ili kuiletea Tanzania medali, ikisisitiza kuwa taifa lina matarajio makubwa kwao.
Akizungumza wakati wa kutembelea kambi ya timu hiyo, Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Oscar Zabron, amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika maandalizi ya timu hiyo na sasa inatarajia kuona matokeo chanya.
“Watanzania wote wanawaangalia. Ushindi mtakaoupata ni ushindi wa Watanzania wote. Tunatarajia mkatuletee medali, hususan dhahabu. Serikali imewagharamia kambi, lishe na mahitaji mengine muhimu, sasa ni wakati wa kupambana,” amesema.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Chama cha Judo Tanzania (JATA), Andrew Mlugu, amesema timu ipo katika hali nzuri baada ya kuweka kambi ya muda mrefu, jambo ambalo halikuwahi kutokea kwa miaka mingi kutokana na changamoto za kifedha.
Amesema wachezaji wana afya njema, morali kubwa na dhamira ya kufanya vizuri katika Michezo ya Jumia ya Madola, huku akiishukuru serikali kwa kutambua umuhimu wa maandalizi ya muda mrefu kwa wanamichezo.
Naye Kocha wa timu ya taifa, Omary Mgoe, amesema timu haikuvunja kambi baada ya kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo ya Afrika, Finland na Junior Arabia, jambo lililosaidia kuboresha kiwango cha wachezaji.
Amesema wachezaji wengi wana uzoefu wa mashindano makubwa ya kimataifa, ikiwemo ya dunia na kufuzu Olimpiki, huku benchi la ufundi likifanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mashindano yaliyopita ili kuongeza ushindani wa timu.
Mlugu amewataka wadau wa mchezo wa judo kuendelea kuiunga mkono timu ya taifa, akieleza kuwa ushirikiano wao utaongeza morali kwa wachezaji na kuisaidia Tanzania kufanya vizuri katika michezo hiyo.




